Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA YA UANDISHI BUNIFU KUJITENGENEZEA AJIRA NA KUKUZA MAARIFA YA TAIFA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ametoa wito kwa waandishi nchini, hususan vijana, kuchangamkia fursa ya uandishi wa vitabu kama njia ya kujitengenezea ajira na kukuza soko la uchapishaji nchini. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa vitabu vya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, Profesa Mkenda alibainisha kuwa uandishi ni suala la msingi kwa maendeleo ya Taifa kwani unasaidia kuhifadhi utamaduni na kuwajenga watoto kuwa Watanzania halisi wanaojitambua kupitia kazi zinazoakisi uzalendo.

Serikali imedhihirisha kuwa uandishi ni kazi inayolipa baada ya kutenga shilingi bilioni moja kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo kiasi cha shilingi milioni 400 kimetumika kuchapa na kusambaza nakala 142,000 za vitabu vya washindi wa tuzo hizo. 

Hatua hii ni fursa kubwa kwa vijana wenye vipaji vya uandishi wa riwaya, ushairi, na hadithi za watoto kuingia katika ushindani huu, kwani serikali imejipanga kununua kazi hizo na kuzisambaza katika shule na maktaba nchini, jambo ambalo linaamsha soko la vitabu na kuwahakikishia waandishi kipato cha uhakika kutokana na kazi zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amesema malengo ya tuzo hizo ni kuibua na kukuza vipaji vipya nchini ili kuongeza upatikanaji wa vitabu bunifu kwa wanafunzi. 

Alieleza kuwa vitabu vilivyozinduliwa tayari vimepata ithibati ya Kamishna wa Elimu, hivyo kusambazwa kwake katika shule zote nchini kutasaidia kuinua kiwango cha usomaji na maarifa kwa watoto. Hii ni nafasi kwa vijana wasomi kutumia kalamu zao kutoa elimu na maarifa yatakayolisaidia Taifa kukua huku wakijitengenezea nafasi za ajira kupitia sekta ya uchapishaji inayozidi kuimarika.

Kupitia tuzo hizi, serikali inakamilisha zawadi ya nne kwa washindi kwa kuwatafutia soko la uhakika, ambapo kila shule itapata wastani wa vitabu 8 hadi 10. 

Hamasa hii inalenga kuwafanya waandishi na wafanyabiashara waone kuwa shughuli ya uandishi na utayarishaji wa vitabu ni sekta yenye tija. Hivyo, vijana wanahimizwa kuachana na mambo yasiyo na tija na badala yake watumie vipaji vyao kuandika kazi zenye ubora zitakazochangia katika mfumo wa elimu na kuongeza hazina ya maarifa ya nchi yetu kwa vizazi vijavyo.

Amezitaka Halmashauri kupanga bajeti kwa umakini ili kuhakikisha shule hazifungwi kutokana na ukosefu wa mahitaji ya msingi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com