Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAMILIKI WA MAGARI SHINYANGA WALALAMIKIA MAFUTA YALIYOCHANGANYWA NA MAJI


@malundeblog

⛽🚧 WAMILIKI WA MAGARI SHINYANGA WALALAMIKIA MAFUTA YANAYODAIWA KUCHANGANYWA NA MAJI 🚦 POLISI NA EWURA WACHUNGUZA👇🏻👉🏿 Wamiliki wa vyombo vya moto waliokwenda kujaza mafuta katika kituo kimoja cha mafuta cha Mjini Shinyanga, wamelalamikia kuwekewa mafuta yanayodaiwa kuchanganywa na maji, hali iliyosababisha magari yao kupoteza nguvu mara baada ya kujaza. https://www.malunde.com/2026/04/Mafuta-Maji.html

♬ original sound - Malunde

Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog

Wamiliki wa vyombo vya moto waliokwenda kujaza mafuta katika kituo kimoja cha mafuta cha Mjini Shinyanga, wamelalamikia kuwekewa mafuta yanayodaiwa kuchanganywa na maji, hali iliyosababisha magari yao kupoteza nguvu mara baada ya kujaza.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 7,2026 baadhi ya wamiliki hao, akiwemo Yona Limo na Adamu Richard, wamesema waligundua hitilafu hizo wakiwa bado hawajaondoka katika kituo hicho, baada ya magari yao kuanza kuonyesha dalili zisizo za kawaida mara tu baada ya kujaza mafuta.

Wamesema hali hiyo iliwalazimu kuanza kufanya uchunguzi wa awali na kubaini uwepo wa maji kwenye mafuta waliyonunua, jambo lililozua hofu kwa watumiaji wengine wa huduma hiyo.

Akizungumza kwa njia ya simu, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa, Karimu Ally, amethibitisha kupokea taarifa hizo na kusema kuwa tayari wanaendelea na uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa madai hayo.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na mamlaka zingine ikiwemo EWURA linaendelea kuchunguza tukio hilo kufuatia malalamiko ya wamiliki wa magari waliodai magari yao kupoteza nguvu baada ya kujaza mafuta katika kituo hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amesema uchunguzi huo unalenga kubaini iwapo mafuta yaliyouzwa yalichanganywa na maji au la, huku wataalamu wa EWURA wakihusishwa moja kwa moja katika uchunguzi huo wa kitaalamu.

Amesema walalamikaji wanahisi mafuta waliyonunua hayakuwa na ubora unaotakiwa, hali iliyosababisha hitilafu za ghafla kwenye magari yao.

Kamanda Magomi amewataka wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea, akisisitiza kuwa majibu sahihi yatatolewa baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kitaalamu.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com