
Na Mbuke Shilagi Kagera.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwassa amemkabidhi rasmi Ofisi Kanali Yahaya Ramadhan Kido leo Februari 13,2026 katika ukumbi wa ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera uliopo Manispaa ya Bukoba.
Akizungumza baada ya makabidhiano Hajjat Fatma Mwassa amesema kuwa Mkoa umefanikiwa kuboresha sekta za huduma zikiwemo sekta za Afya na Elimu.
Amesema kuwa katika Halmashauri zote saba za Mkoa wa Kagera tayari zipo hospitali za Wilaya ambapo zote zinatumika.
Aidha amemuomba Rc Kanali Kido kutupia jicho la karibu katika hospitali ya Wilaya ya Muleba kutokana na changamoto ya mkandarasi na ubora wa ujenzi.
Akipokea rasmi ofisi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Yahaya Ramadhani Kido amesema kuwa kwa kuwa Mkoa wa Kagera upo mpakani hivyo suala la ulinzi na usalama litakuwa ni kipaumbele namba moja katika Taifa na katika uongozi wake.
"Nitashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuendeleza kwa kuendelea kuimarisha usalama kwakua Mkoa wetu unapakana na Nchi jirani", amesema RC Kanali Kido.
Aidha ameongeza kuwa atasimamia miradi yote inayoendelea kutekelezwa na ile inayopangwa kutekelezwa ili iendane na thamani ya fedha zilizotolewa na serikali na kukamilika kwa wakati.
Amesema kuwa amepokea rasmi dhamana ya uongozi ya Mkoa huo akiwa na dhamira thabiti ya kuendeleza yaliyofanywa na mtangulizi wake na yale yote yaliyoelezwa na Mkuu wa Mkoa mstaafu Hajat Fatma Mwassa yatafatiliwa kwa kina na kuhakikisha yanakamilika kwa wakati.




Social Plugin