-Hatua yachukuliwa baada ya kushindwa kudhibiti vumbi na kutotekeleza maelekezo ya baraza
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekifungia Kiwanda cha JUYE Concrete Ltd kilichopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam, kwa kushindwa kuzingatia sheria za mazingira na kusababisha uchafuzi wa hewa unaotokana na vumbi.
Akizungumza mara baada ya kufungwa kwa kiwanda hicho leo Februari 12, 2026 Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria wa NEMC, Hamad Taimul, amesema JUYE Concrete Ltd imepewa maelekezo mara kadhaa ya kuweka mifumo ya kuzuia vumbi lisitoke nje ya eneo la uzalishaji, lakini haikuyatekeleza.
“Tumewabembeleza kwa muda wa mwaka mzima. Tumewaelekeza mara tano kutengeneza mfumo wa kudhibiti vumbi ili lisienee kwenye makazi ya wananchi, lakini hawajatekeleza,” amesema Taimul.
Amesisitiza kuwa NEMC inaunga mkono maendeleo ya viwanda kutokana na mchango wake kwa uchumi wa taifa kupitia kodi na ajira, lakini afya na usalama wa wananchi haviwezi kuachwa nyuma.
“Tunatambua umuhimu wa viwanda, lakini uhai wa watu ni muhimu zaidi. Mnatengeneza bidhaa kwa ajili ya wananchi; kama shughuli zenu zinaathiri afya zao, hizo bidhaa mtamuuzia nani?” Amesema .
Kwa mujibu wa Taimul, hatua ya kufungia kiwanda hicho inalenga kutoa nafasi kwa uongozi wa JUYE Concrete kufanya marekebisho muhimu, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya kudhibiti vumbi.
“Tumesimamisha uzalishaji ili wapate muda wa kufanya maboresho. Wakikamilisha, tutakuja kukagua na kufungua uzalishaji,” ameongeza.
Aidha amesema kuwa NEMC imekuwa ikipokea malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wakazi wa maeneo jirani kuhusu vumbi linalotokana na shughuli za uchanganyaji wa zege, hali inayodaiwa kuathiri mazingira na afya.
Social Plugin