Mkurugenzi Mtendaji wa Equity For Tanzania Limited- EFTA Bwana Nicomed Bohay akizungumza na wageni waalikwa wakati wa uzindunzi wa Hati Fungani za EFTA tukio lilofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam katika Hotel ya Kilimanjaro Hyatt Regency.
Wageni mbalimbali, wakiwemo wadau wa sekta ya fedha, wawekezaji na wawakilishi wa taasisi za kifedha, wakifuatilia kwa makini tukio la uzinduzi wa EFTA Corporate Bond ya Shilingi bilioni 50, lililofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo uliashiria hatua mpya ya kuimarisha upatikanaji wa mtaji wa muda mrefu kwa sekta za uzalishaji nchini.
Wajumbe wa jopo la majadiliano wakichangia mada wakati wa uzinduzi wa EFTA Corporate Bond ya Shilingi bilioni 50 jijini Dar es Salaam, wakijadili umuhimu wa mtaji wa muda mrefu katika kuimarisha sekta za uzalishaji na kukuza masoko ya mitaji nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Nicomed Bohay, akichangia mjadala wa jopo wakati wa uzinduzi wa Hati Fungani ya Sh bilioni 50 jijini Dar es Salaam, akieleza namna mpango huo unavyolenga kuimarisha mtaji wa muda mrefu kwa sekta za uzalishaji na kutoa fursa ya uwekezaji kwa umma.



Wageni mbalimbali, wakiwemo wadau wa sekta ya fedha, wawekezaji na wawakilishi wa taasisi za kifedha, wakifuatilia kwa makini tukio la uzinduzi wa EFTA Corporate Bond ya Shilingi bilioni 50, lililofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo uliashiria hatua mpya ya kuimarisha upatikanaji wa mtaji wa muda mrefu kwa sekta za uzalishaji nchini.

Muhumiza Buberwa, Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa Benki ya CRDB, akizungumza wakati wa uzinduzi wa EFTA Corporate Bond jijini Dar es Salaam, akieleza umuhimu wa ushirikiano kati ya benki na masoko ya mitaji katika kuimarisha ufadhili wa sekta za uzalishaji nchini.
Mkuu wa Idara ya Fedha -EFTA Edward Mamaneki akitoa taarifa kwa wageni waalikwa kuhusu namna ambavyo hati fungani ilivyoundwa .

Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu na Sheria wa Equity for Tanzania Limited (EFTA), Lucy Bwana, akifuatilia kwa makini uzinduzi wa EFTA Corporate Bond ya Shilingi bilioni 50 uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam, tukio lililolenga kuimarisha upatikanaji wa mtaji wa muda mrefu kwa sekta za uzalishaji nchini.



.jpeg)
Wafanyakazi wa Equity for Tanzania Limited (EFTA) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi rasmi wa EFTA Corporate Bond ya Shilingi bilioni 50 jijini Dar es Salaam, wakionesha mshikamano na dhamira ya kuimarisha ufadhili wa muda mrefu kwa sekta za uzalishaji nchini.
MSUKUMO MPYA SEKTA ZA UZALISHAJI ,EFTA YAWEKA BILIONI 50 HATI FUNGANI
Na Mwandishi wetu -Dar es Salaam .
Katika mijadala mingi kuhusu maendeleo ya uchumi wa Tanzania, hoja ya upatikanaji wa mtaji imeendelea kujitokeza kama kikwazo kikubwa kwa sekta za uzalishaji.
Wakulima wanahitaji mitambo, wafanyabiashara wanahitaji magari ya usafirishaji, na viwanda vidogo vinahitaji mashine za kuongeza thamani ya bidhaa.
Changamoto si ukosefu wa fursa — bali ni ukosefu wa mtaji wa muda mrefu unaoendana na mahitaji hayo.
Ni katika muktadha huo ambapo Kampuni ya Equity for Tanzania Limited (EFTA) imezindua Hati Fungani ya Kampuni yenye thamani ya Shilingi bilioni 50, hatua inayotajwa kuwa ya kimkakati katika kuimarisha ufadhili wa sekta za uzalishaji kupitia masoko ya mitaji.
Uzinduzi huo uliofanyika tarehe 10 Februari 2026 katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam uliwakutanisha wadau wa sekta ya fedha, wawekezaji na taasisi za kifedha, huku ukifungua mjadala mpana kuhusu nafasi ya masoko ya mitaji katika kukuza uchumi halisi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Nicomed Bohay, dhamira kuu ya mpango huo ni kuoanisha mtaji wa muda mrefu na mali zinazozalisha mapato kwa muda mrefu.
“Tunafadhili mali kama matrekta, magari ya biashara na mitambo ya viwandani ambayo huzalisha mapato kwa miaka kadhaa. Ili sekta hizi zikue kwa uthabiti, zinahitaji mtaji wa muda mrefu unaolingana na maisha ya mali hizo,” alisema Bohay.
Fedha zitakazokusanywa zitaelekezwa moja kwa moja katika sekta kama kilimo, usafirishaji, ujenzi, madini na uchakataji wa mazao.
Kinachovutia zaidi katika toleo hili ni kiwango cha riba cha asilimia 14 kwa mwaka — kiwango ambacho kimetajwa kuwa cha juu na chenye ushindani mkubwa katika soko la hati fungani za kampuni nchini.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa masoko ya mitaji, hii ni mara ya kwanza kwa hati fungani ya kampuni katika soko la ndani kutolewa kwa kiwango hicho cha riba, hatua inayotarajiwa kuvutia wawekezaji wanaotafuta mapato ya juu ndani ya mfumo uliodhibitiwa.
“Tumezingatia hali ya soko pamoja na uimara wa jalada la mali tunazofadhili. Riba ya asilimia 14 inaakisi thamani tunayoitoa kwa wawekezaji huku tukihakikisha uendelevu wa biashara,” alisema Bohay.
Kwa wawekezaji, kiwango hicho kinaweka alama mpya katika ushindani wa bidhaa za mapato ya kudumu (fixed income), hasa katika kipindi ambacho wawekezaji wengi wanatafuta mbadala wenye mapato bora.
Prof. Andrew Temu, mchumi wa kilimo, Mwenyekiti Mtendaji wa Diligent Consulting na aliyewahi kuwa Mhadhiri Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), alisema upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu ni msingi wa mageuzi ya uzalishaji.
“Afrika haina tatizo la uhitaji wa vifaa vya uzalishaji; changamoto ni namna ya kuvipata. Mtaji wa muda mrefu unazipa taasisi uwezo wa kusaidia wakulima na wajasiriamali kuongeza uzalishaji na mapato,” alisema Prof. Temu.
Kwa maoni yake, masoko ya mitaji yanaweza kuwa daraja muhimu la kuunganisha akiba za ndani na mahitaji ya uzalishaji.
Kwa upande wake, Meneja wa Maendeleo ya Soko kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), David Magabe, alisema ushiriki wa taasisi kama EFTA unaonyesha kukua kwa soko la mitaji nchini.
“Utoaji wa hati fungani zenye mvuto kama hizi unaongeza chaguzi za uwekezaji na kusaidia kuelekeza mtaji kwenye sekta za uzalishaji. Hii ni ishara ya soko linalokua na kukomaa,” alisema Magabe.
Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa Benki ya CRDB, Muhumiza Buberwa, alisema ushirikiano kati ya benki na taasisi za masoko ya mitaji unaongeza uimara wa mfumo wa kifedha.
“Kupitia masoko ya mitaji, tunaona fursa ya kupanua vyanzo vya mtaji na kusaidia sekta halisi za uchumi.
Hii inachochea ajira na ukuaji wa biashara,” alisema Buberwa. Kwa ujumla, Hati Fungani ya EFTA inaonekana kuwa zaidi ya chombo cha kukusanya mtaji.
Kwa kiwango cha riba cha asilimia 14, na muundo wa senior secured, mpango huu unaunganisha matarajio ya wawekezaji wa mapato ya juu na mahitaji ya sekta za uzalishaji zinazohitaji mtaji wa muda mrefu. Katika uchumi unaokua na unaohitaji mitaji ya uvumilivu, hatua hii inaweza kuwa mfano wa jinsi masoko ya mitaji yanavyoweza kuwa kichocheo cha mageuzi ya uzalishaji nchini.
Mwisho



Social Plugin