Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAPUNGUZA ADA ZA USAJILI WA VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI; MWANA FA AAGIZA MALIPO YA WAFANYAKAZI YASHUGHULIKIWE NDANI YA WIKI MOJA



Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Serikali imepunguza kwa kiasi kikubwa ada za maombi ya leseni kwa vyombo vya habari mtandaoni, kutoka shilingi laki tano hadi 50,000=  huku ada ya maombi ikiwa shilingi 10,000/= tu  kutoka shilingi 50,000/=— hatua inayotajwa kuwa mkombozi kwa wanahabari na wamiliki wa blog nchini.

Hatua hiyo imetangazwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma.

Mbali na kupunguza ada hizo, Mwinjuma ameielekeza TCRA kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha wafanyakazi wa vyombo vya habari wanalipwa stahiki zao kwa wakati, wakiwemo wale wanaodai mishahara ya zaidi ya miezi mitano.

Amesisitiza kuwa ndani ya wiki moja anatarajia kupokea mrejesho wa hatua zilizochukuliwa kuhusu suala hilo.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi kwa vyombo vya habari, huku akisisitiza umuhimu wa ubora wa maudhui, kuzingatia maadili ya taaluma na kulinda haki miliki.

“Haki ya kupata taarifa ni ya kila Mtanzania, hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuwafikia wananchi wote bila upendeleo,” amesisitiza.

Aidha, amesema wizara itaendelea kuimarisha mazingira ya sekta hiyo ili wananchi wa vijijini wanufaike na huduma za utangazaji kwa urahisi, sambamba na kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Unde (AI) kwa tija.

Katika hatua nyingine, Mwinjuma ameielekeza Kampuni ya Usambazaji wa Machapisho na Vifaa vya Utangazaji (KOSOTO) kushirikiana na TCRA kupambana na waharamia wa maudhui na kuwasilisha mrejesho ndani ya mwezi mmoja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri, ametaja takwimu za vyombo vya habari vilivyosajiliwa nchini na kuahidi kuendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano kwa kuzingatia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Mkutano huo wa siku mbili, unaofanyika Februari 12 na 13, 2026, umewakutanisha viongozi na wadau wa sekta ya utangazaji kujadili namna ya kuimarisha na kupanua huduma za utangazaji nchini.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com