
Ofisi ya RAS Singida, ikiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Bi. Fatuma Mganga, imepokea na kushiriki katika mjadala wa kupinga ukatili wa kijinsia (GBV) uliowahusisha wadau mbalimbali pamoja na jamii kwa ujumla, kwa lengo la kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo hivyo mkoani hapa.
Akizungumza katika kikao hicho, Bi. Mganga alisema dhana ya ukatili wa kijinsia inapaswa kuangaliwa kwa kuzingatia uzoefu wa zamani sambamba na mabadiliko ya sasa katika jamii. Alieleza kuwa kadri nyakati zinavyobadilika, ndivyo pia aina za ukatili zinavyojitokeza kwa sura mpya, hivyo kunahitajika umakini na mikakati madhubuti ya kukabiliana nayo.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuenzi mila na desturi zenye tija kwa jamii badala ya kuzikataa moja kwa moja na kuiga tamaduni za nje bila kuchuja yaliyo mema. Alitoa wito kwa jamii kuimarisha mshikamano wa familia, kuweka mizani kati ya mila na mabadiliko ya kisasa, na kutambua kuwa mila bora ni msingi wa maadili na ustawi wa jamii.
Katika ziara hiyo, timu ilitembelea Shule ya Msingi ya Wasichana Ikungi, shule jumuishi inayohudumia wanafunzi wenye ulemavu mbalimbali, wakiwemo wasioona, wenye uoni hafifu, wenye ualbino na wenye ulemavu wa viungo. Shule hiyo pia ina walimu kutoka katika jamii ya watu wenye ulemavu. Wanafunzi wenye ulemavu wanaishi shuleni, huku wale wasio na ulemavu wakiishi majumbani.
Pamoja na uwepo wa teknolojia saidizi kama mashine za breli, bado kuna upungufu wa vifaa hivyo. Shule ina Klabu ya Shule Salama (Gender Club) na walimu waliobobea katika elimu maalum. Wanafunzi walionesha uelewa mzuri kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia na mbinu za kujilinda dhidi ya vitendo hivyo.
Ziara hiyo iliendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Ikungi, ambapo wanafunzi wengi wenye umri kati ya miaka 13 hadi 19 walishiriki kikamilifu katika mjadala. Walionesha uelewa wa masuala ya ukatili wa kijinsia, hususan ukatili wa kingono, na walikuwa tayari kueleza changamoto zao walipopewa fursa salama ya kufanya hivyo.
Timu hiyo iliambatana na Afisa Ustawi wa Jamii aliyeshughulikia masuala nyeti kwa weledi, akihakikisha watoto wanahisi kusikilizwa, kulindwa na kuthaminiwa.
Katika Soko la Muhunze, changamoto zilizobainishwa zilihusu zaidi matunzo ya watoto, migogoro ya mirathi na ardhi, pamoja na vitendo vya ukatili wa kimwili vinavyotokana na unywaji wa pombe kupita kiasi, ambapo baadhi ya wanaume hurudi nyumbani na kuwafanyia wake zao vitendo vya ukatili.




Social Plugin