Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BIMA YA MAZAO TABORA: MATUNDA YA COP30 KUIMARISHA KILIMO STAHIMILIVU



Na Hadija Omary Mazezele - Tabora

SAFARI ya Tanzania kuelekea mapinduzi ya kilimo stahimilivu imepata msukumo mpya kufuatia Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) uliomalizika Novemba 21, 2025, nchini Brazil kuanza kutoa matumaini kwa wakulima wa tumbaku mkoani Tabora. 

Katika mkutano huo, Tanzania imefanikiwa kupata ahadi ya awali ya dola za Kimarekani milioni 20 sawa na shilingi bilioni 48 za kitanzania kutoka kutoka Mfuko wa Hasara na Uharibifu (Loss and Damage Fund).

Fedha hizo zimeelekezwa mahususi katika miradi miwili ya kimkakati, ukiwemo uanzishwaji wa bima za kilimo zinazoendana na mabadiliko ya hali ya hewa. 

Ripoti ya Benkli ya Dunia (WB) "Tanzania Country Climate and Development Report (CCDR)", ya mwaka 2022 inakakadiria kuwa, ifikapo mwaka 2030, Tanzania inaweza kupoteza kati ya asilimia moja hadi mbili ya Pato la Taifa (GDP) kila mwaka kutokana na athari za hali ya hewa katika kilimo.

Mbali na hayo, takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Bodi ya Tumbaku Tanzania na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kati ya mwaka 2022 na 2023, zinaashiria hali ya hatari kwa wakulima. 

Ripoti hizo zinabainisha kuwa mvua zisizo tabirika zinasababisha kushuka kwa ubora wa majani ya tumbaku, jambo linalochangia kuporomoka kwa bei katika soko la dunia na kusababisha upotevu wa mapato.


Hivyo mpango wa bima kilimo unalenga kuwa kinga ya kipato kwa wakulima wadogo dhidi ya majanga ya asili kama ukame na mafuriko yanayoweza kuharibu mazao yao.
Hali hiyo imeanza kudhihirika kwa vitendo mkoani Tabora, ambapo zoezi la usajili wa bima ya mazao kwa wakulima wa tumbaku linaendelea kushika kasi.

 Katika wilaya za Tabora Manispaa, Uyui, na Nzega, takriban wakulima 5,900 tayari wameshasajiliwa, huku kukiwa na lengo la kuwafikia wakulima 14,000 katika wilaya hizo na zaidi ya 50,000 katika mkoa wote wa Tabora.

Kaimu Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Consolata Kiluma, amewahimiza wakulima kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika bima hiyo na kufafanua kuwam kuwa usajili huo utasaidia serikali kupata makisio sahihi ya pembejeo, huku mipango ya kuanzisha Bima ya Afya na Fao la Uzalishaji kwa wakulima ikiendelea kupikwa.

Kwa upande wake, Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Tabora, Venance Msafiri, amefafanua kuwa bima hizo ni mkombozi katika kuimarisha vyama vya ushirika hasa kuwalinda wanachama wake amba oni wakulima dhidi ya majanga ya asili.

Amesema mfumo huo utasaidia kumtambua mkulima mmoja mmoja, changamoto zake, na kuhakikisha anafikia masoko kwa usalama zaidi.

Zainabu Athumani, mkulima kutoka Combanio AMCOS, anaelezea faraja yake akisema kuwa bima hiyo imekuja wakati muafaka.

“Nimeupenda mfumo huu kwani unapata janga kama la mvua kubwa inayoharibu mazao, bima itanisaidia kusimama tena imara bila kuanguka kiuchumi,” anasema Zainabu.

Naye Hussein Rashid, mkulima mwingine wa tumbaku, (maeneo gani) ameipongeza serikali kwa hatua hiyo akisema ukosefu wa bima huko nyuma ulikuwa unawarudisha nyuma kimaendeleo kila wanapopatwa na majanga ya hali ya hewa.

Ushiriki wa Tanzania katika COP30 umeanza kuleta matokeo chanya yanayomgusa moja kwa moja mwananchi wa chini, badala ya kubaki kwenye meza za majadiliano nchini Brazil, maamuzi hayo sasa yanatafsiriwa kuwa suluhu za kimaisha kwa wakulima wa Tabora.

Utekelezaji wa miradi hii ni dhihirisho kuwa rasilimali zinazopatikana kimataifa zinaweza kuimarisha ustahimilivu wa taifa dhidi ya hasara na uharibifu.

Endapo jitihada hizi zitasimamiwa kwa ufanisi na uaminifu, COP30 itakumbukwa kama kichocheo kikubwa cha kulinda uchumi wa wakulima na kuhakikisha usalama wa chakula na kipato kwa wakulima mkoani Tabora na nchini kote.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com