
Na Hadija Omary Mazezele
Katika nyakati hizi za mabadiliko ya tabianchi, kilimo kinahitaji mbinu bunifu na endelevu, hasa kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi (Climate-Smart Agriculture), ili kusaidia kuongeza uzalishaji, kulinda mazingira na kuongeza ustahimilivu wa wakulima dhidi ya athari za ukame, mafuriko na mabadiliko ya misimu ya mvua.
Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa muhimu ya kilimo nchini Tanzania, ukijulikana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara yanayochangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Tabora huzalisha mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, mtama, uwele, mihogo na kunde, pamoja na mazao ya biashara kama tumbaku, alizeti, pamba na karanga.
Tovuti rasmi ya serikali mkoa wa Tabora (RS Tabora) Ripoti ya shughuli za kiuchumi ya mwaka 2024/2025 na Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuhusu wasifu wa pato la mkoa (GDP Regional Profiles) ya mwaka 2024, zinaeleza kuwa asilimia 70 ya pato la mkoa wa Tabora linatokana na kilimo na ufugaji kutokana na kuwa na utajiri wa rasilimali ardhi.
Licha ya utajiri huu wa rasilimali ardhi na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo, wakulima wa Tabora bado wanazalisha kwa tija ndogo kutokana na changamoto kadhaa za kimfumo na kimazingira.
Changamoto kubwa inayowakabili wakulima wa Tabora ni kutofahamu afya ya udongo jambo ambalo lingewasaidia kujua eneo gani apande mazao gani na atumie mbolea ya aina gani kwa kiwango gani.
Changamoto nyingine mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha mvua kunyesha kwa kuchelewa, kukatika kwa msimu wa mvua au kunyesha kwa kiwango kisichotabirika. Hali hii huathiri uzalishaji wa mazao kama mahindi, mpunga na tumbaku ambayo hutegemea mvua za uhakika.

Baadhi ya wakulima katika kijiji cha Chang’ombe, kata ya Ndevelwa, manispaa ya Tabora, wameeleza namna ambavyo mabadiliko ya tabianchi huwaathiri, ambapo wakati mwingine hujikuta wakipanda mara mbili au zaidi bila mafanikio, hali inayowasababishia hasara na kuwakatisha tamaa.
Mmoja wa wakulima hao Asha Rajabu amesema mabadiliko ya tabianchi yamekifanya kilimo kuwa shughuli isiyokuwa na uhakika kwa mkulima.
Katika Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), uliofanyika nchini Brazil, kilimo kilipewa kipaumbele kama sekta muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Nchi hizo, ikiwemo Tanzania ziliazimia na kupitisha mikakati ya kilimo kinachozingatia tabianchi (Climate-Smart Agriculture) kwa kutumia sensa, droni na mifumo ya Akili Unde (AI) kufuatilia rutuba ya udongo na matumizi ya maji.
Azimio hilo pamoja na mambo mengine linalenga kuwawezesha wakulima kufahamu afya ya udongo ili wafanye maamuzi sahihi ya aina ya mazao wanayoweza kupanda au aina gani ya mbolea itumike kwa kiasi gani, badala ya kilimo cha mazao.
Katika kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa nguzo kuu ya maendeleo ya taifa, hasa kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, Halmashauri ya Mji wa Nzega mkoani Tabora imeanza zoezi la upimaji ardhi ili kubaini rutuba ya udongo, matumizi sahihi ya pembejeo na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nzega, Mwarami Seif, amesema upimaji wa afya ya udongo utasaidia kubaini ni aina gani ya mazao yapandwe ili kuendana na mabadiliko ya tabianchi, zoezi ambalo serikali imebeba gharama zote ambapo mkulima hatalipa kiasi chochote cha fedha.
“Upimaji wa udongo ni sawa na ramani ya hazina ya mkulima kwa kuwa, humsaidia kujua kiasi halisi cha mbolea kinachohitajika, hivyo kumpunguzia gharama ya kununua mbolea nyingi ambazo udongo hauhitaji, anapata uhakika kama udongo wa shamba lake unafaa kwa Mahindi, Muhogo au Mpunga, hivyo kupunguza hatari ya mazao kunyauka au kutoa mavuno duni,” alisema Seif.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2019, kuhusu tija ya kilimo nchini Tanzania, wakulima wadogo wanazalisha chini ya asilimia 40 ya uwezo halisi wa ardhi yao kutokana na kutojua mahitaji ya udongo.
Kwa upande wake Ripoti ya FAO kuhusu Hali ya Rasilimali za Ardhi na Maji Dunianiya mwaka 2021, inabainisha kuwa karibu asilimia 30 hadi 50 ya mbolea inayotumika barani Afrika inapotea kwa sababu inatumiwa kwenye udongo wenye asidi (pH) isiyo sahihi, hivyo mimea haiwezi kuitumia.
Mhandisi Juma Mdeke, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo amesema udongo uliopimwa na kuboreshwa una uwezo mkubwa wa kuhifadhi unyevu wakati wa ukame.
“Mazao yaliyo kwenye udongo wenye afya hustahimili kwa muda mrefu kuliko yale ya kwenye udongo uliokauka virutubisho, hivyo ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni muhimu kupima afya ya udongo,” alisema.
Amebainisha kuwa, mbali na kupima udongo wakulima wataelimishwa na kupewa ushauri ili kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa bora, endelevu na yenye tija.
Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa katika ripoti yake yam waka 2022, udongo uliopoteza afya huzalisha mazao yasiyo na virutubisho kama Zinc, Iron, Iodine, hivyo kusababisha tatizo la udumavu ambalo nchini Tanzania limefikia 32% kwa watoto chini ya miaka mitano.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakulima wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo ya serikali ya kupima afya ya udongo kwani itawasaidia kuondokana na changamoto zinazowakabili na badala yake itaongeza tija ya uzalishaji na kukuza kilimo.
Kwa upande wake Zinabu Athumani ambaye ni mkulima kutokaCombanio AMCOS ameeleza namna zoezo zoezi hilolilivyokuwa bora kwao na limekuja muda mzuri litakalosaidiauendelevu wa shamba,kilimo na maisha ya familia yake.
“mfumo huu mie nimeupenda kwani unaweza pata janga la mvuo na kupelekea kuharibu mazao hivyo kupitia Bima nawezasaidika na nikaendelea kusimama imara kwenye kilimo”amesema Zainabu.
Kwa upande wake Hussein Rashid ambaye ni mkulima waTumbaku amepongeza hatua hiyo ya serikali huku akibainishachangamoto walizokuwa wakizipata kutokana na kutokuwa naBima hizo za mazao akifafanua upotevu waliokuwa wakiupatahali iliyokuwa ikiwarudisha nyuma katika mfumo mzima wakilimo na kiuchumi.
Hata hivyo, kuleta mageuzi ya kweli ya kiuchumi mkoani Tabora kunategemea namna sekta ya kilimo itakavyofanyiwa maboresho ya kimkakati.
Mkazo unapaswa kuwekwa katika uwekezaji wa pembejeo za kisasa, huduma za ugani, na miundombinu ya umwagiliaji, sambamba na mifumo imara ya bima na masoko. Bila hatua hizi madhubuti, jasho la mkulima wa Tabora litaendelea kupotea kutokana na changamoto za kimazingira na kuyumba kwa soko.
Social Plugin