
Na Hadija Omary Mazezele
Katika Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) uliofanyika nchini Brazil, Tanzania ilisimama kidete si tu kama mshiriki, bali pia kama kiongozi wa msimamo wa Afrika.
Ikiwa Mwenyekiti wa Kikundi cha Majadiliano cha Afrika (AGN), Tanzania ilisisitiza umuhimu wa huduma za hali ya hewa, sera jumuishi na mifumo ya chakula endelevu kama nguzo kuu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima.
Msimamo wa Tanzania, kama mwakilishi wa bara la Afrika, ni kwamba huduma za hali ya hewa ni muhimu kwa kuwasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi kuhusu kilimo, hasa katika mazingira ya sasa yanayobadilika kwa kasi.
Kauli ya Tanzania, iliyotolewa na Dkt. Richard Mayungi Mshauri wa Rais kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi na mwenyekiti wa AGN, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, wakati wa COP30, ilisisitiza umuhimu wa huduma za hali ya hewa kuwafikia wakulima wadogo ambao ndio walio hatarini zaidi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wakulima wadogo nchini wakiwemo wa mkoa wa Tabora hupoteza mapato, usalama wa chakula na ustawi wa kijamii kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa taarifa sahihi za hali ya hewa.
Tafiti zinaonyesha kupungua kwa mavuno kwa zaidi ya asilimia 30–50, kushuka kwa kipato cha kaya kwa asilimia 60–80, na kuongezeka kwa hatari ya umasikini na uhamaji wa kijamii.
Ripoti ya Taasisi ya utafiti na uchambuzi wa sera za kiuchumi na kijamii nchini (ESRF) kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima wadogo ya mwaka 2013 ilibainisha kuwa, wakulima wadogo hupoteza sehemu kubwa ya mavuno kutokana na ukame na mvua zisizotabirika, hali inayosababisha upungufu wa chakula na kipato vijijini.
Ripoti ya Benki ya Duinia (WB) kuhusu athari za kicuhumi zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ya mwaka 2024, ilionyesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusababisha watu milioni 13 kuhamishwa ndani ya nchi kutokana na ukame na mafuriko barani Afrika.
Kulingana na Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2023, ilionyesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yameongeza migogoro kati ya wakulima na wafugaji, na kuathiri haki za kijamii na kiuchumi, huku shirika la IIrish Aid katika ripoti yake ya mwaka 2018 ilibainisha kuwa kupungua kwa mavuno husababisha lishe duni, hususan kwa watoto na wanawake.
Kutamatika kwa mkutano wa COP30 kumeendelea kuibua maswali na mijadala kwa wakulima wa mkoa wa Tabora na nchini kwa jumla, kuhusu huduma za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), hususan taarifa zinazohusu mienendo ya mvua na ukame.
Kwa mujibu wa Kidumila Mtandi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chang’ombe katika wilaya ya Tabora mkoa wa Tabora, mavuno yake yameshuka kutoka gunia 80 hadi gunia tano.
Hii ni taswira ya athari binafsi, huku tafiti za kitaifa zikionyesha upungufu wa mavuno kwa asilimia 30–50 na kukiosekana kwa taarifa sahihi za hali ya ewa kumechangia hali hiyo.
Anasema huwa anasikia taarifa za hali ya hewa zikitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) kupitia redio, lakini mara anashindwa kuelewa kutokana na lugha inayotumika jambo linalomfanya mtandi na wakulima wrngine wa Tabora kulima kwa mazoea hivyo kupata hasara kwenye mavuno.
“Wapo wananchi hapa kijijini hawana redio wala simu janja, hivyo kushindwa kufuatilia taarifa hizo. Hali hii imekuwa kikwazo kwa wakulima wengi kufikia malengo yao ya kilimo kutokana kukosa taarifa sahihi za hali ya hew ana kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Ameongeza kuwa, miaka sita iliyopita alikuwa na uwezo wa kupata hadi gunia 80 za mahindi na gunia 100 za mpunga pamoja na mazao mengine, lakini kwa sasa hupata gunia tano za mahindi na gunia nane za mpunga.
Kwa upande wake, Asha Masoud ambaye pia ni mkulima wa Kijiji cha Chang'ombe ameiomba TMA iwe na mpango madhubuti wa kuwasilisha taarifa za hali ya hewa kwa wakulima kwa lugha rahisi na inayoeleweka.
“Kufanya hivyo kutasaidia wakulima kupata taarifa sahihi kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata na vijiji kuhusu mwelekeo wa mvua,” amesema.
Naye Eliud John, mkulima wa mazao ya chakula, amesisitiza na kuomba maafisa ugani wapate nafasi ya kuwatembelea wakulima na kutoa ufafanuzi badala ya kukaa ofisini.
Amesema kufanya hivyo kutawasaidia wakulima kuamua aina ya mazao ya kulima na kuepuka hasara.
Hata hivyo, mjadala wa COP30 umefungua ukurasa mpya kwa Tanzania katika kuimarisha juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan katika sekta ya kilimo inayogusa maisha ya wananchi wengi vijijini.
Kupitia msimamo wa Tanzania kama kinara wa masuala ya Afrika, imebainika wazi kuwa huduma za hali ya hewa zilizo sahihi, za wakati na zinazoeleweka kwa wakulima ni nguzo muhimu za kujenga kilimo chenye ustahimilivu.
Changamoto zinazowakumba wakulima wa mkoa wa Tabora, ikiwemo kukosekana kwa taarifa za uhakika za hali ya hewa na mifumo hafifu ya mawasiliano, zinaakisi uhalisia unaohitaji hatua za haraka na za kimkakati.
COP30 imeweka msingi wa uwajibikaji kwa serikali, taasisi za hali ya hewa na wadau wa maendeleo kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinawafikia wakulima wote kwa lugha rahisi na njia zinazowafikia.
Hatua hizi si tu zitapunguza hasara ya mazao, bali pia zitachangia kuongeza uzalishaji, usalama wa chakula na ustawi wa wananchi.
Msimamo wa Tanzania katika COP30 unagusa moja kwa moja wakulima wadogo kama wa Tabora, ambao wanakabiliana na changamoto hizi kila siku.
Kwa wakulima kama Kidumila, taarifa sahihi za hali ya hewa zinaweza kubadilisha maamuzi shambani na kuleta mavuno bora.
Social Plugin