
Wakazi na wajasiriamali wa mkoa wa Pwani wametoa wito wa dhati kwa Watanzania wote kuilinda amani ya nchi kwa gharama yoyote wakibainisha kuwa utulivu ndio nguzo kuu inayowezesha shughuli za maendeleo kufanyika bila vikwazo.
Maria Mvulla ambaye ni mkazi na mjasiriamali wa Maili Moja wilayani Kibaha amesisitiza kuwa amani ni tunu inayopaswa kulindwa kwa kuepuka mihemko ya aina yoyote kwani machafuko yakitokea pato la taifa litashuka na gharama ya kuirejesha amani hiyo itakuwa kubwa sana kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Alieleza kuwa mshikamano uliopo sasa bila ubaguzi wa aina yoyote ndio siri ya utulivu wa Tanzania hivyo kuna kila sababu ya kudumisha umoja huo kwa ajili ya ustawi wa wote.
Kwa upande wake Francis Kalimba ambaye pia ni mkazi wa Maili Moja ameeleza imani yake kuwa amani ya Tanzania bado ni imara na inapaswa kutunzwa kwa hali na mali ili kuzuia kundi dogo la watu wasioitakia mema nchi wasiweze kuivuruga.
Aliongeza kuwa Watanzania wana amana kubwa ya mshikamano ambayo inapaswa kulindwa kwa nguvu zote kwani ndiyo inayotofautisha nchi hii na maeneo mengine yaliyokumbwa na migogoro inayozuia wananchi kufurahia haki na maisha yao ya kila siku.
Naye Mohamed Mpoto mkazi wa Picha ya Ndege wilayani humo amefafanua kuwa amani ndio chanzo kikuu cha maendeleo na bila uwepo wake hakuna hatua yoyote ya kiuchumi inayoweza kupigwa na mtu binafsi au taifa kwa ujumla.
Amewasihi Watanzania kuwa na mshikamano wa pamoja na utulivu wa hali ya juu ili kila mwananchi aweze kuendelea na shughuli zake za kujiingizia kipato na ujenzi wa taifa bila hofu yoyote. Maoni ya wakazi hawa yanakuja kama sehemu ya sauti za wananchi zinazosisitiza umuhimu wa amani katika kipindi hiki ambacho serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama ili kukuza mnyororo wa thamani wa uchumi wa nchi.
Social Plugin