Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA NA SERBIA ZAJADILI USHIRIKIANO WA AJIRA NA MAENDELEO YA RASILIMALI WATU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu akisalimiana na Waziri wa Kazi, Ajira na Ustawi wa Jamii wa Serbia, Mhe. Milica Djurdjevic, walipo kutana katika kikao cha pembeni (side meeting) kujadili ushirikiano wa masuala ya Kazi na Ajira, Jijini Riyadh, Saudi Arabia.

************

Tanzania na Jamhuri ya Serbia zimejadili fursa za kuimarisha ushirikiano wa masuala ya kazi, ajira na maendeleo ya rasilimali watu, hususan katika Sekta ya Ujenzi na maeneo mengine muhimu ya kiuchumi.

Hayo yamebainishwa wakati wa kikao cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu na Waziri wa Kazi, Ajira na Ustawi wa Jamii wa Serbia, Mhe. Milica Djurdjevic Stamenkovski, walipokutana katika Mkutano wa Mawaziri wa Kazi Duniani (Global Labour Market Conference) uliofanyika Jijini Riyadh, Saudi Arabia.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Sangu amesema Serikali ya Tanzania imeendelea kufanya mageuzi makubwa yanayolenga kukuza ajira zenye staha, kuongeza ujuzi kwa nguvu kazi na kupanua fursa za ajira kwa wananchi.

Vilevile, Mhe. Sangu alitumia fursa hiyo kueleza wataalamu na uwezo wa wafanyakazi katika nyanja mbalimbali zikiwemo uhandisi, afya, elimu, uhasibu, utawala wa biashara, uchumi, sheria, utalii na ukarimu, kilimo, TEHAMA, biashara ya kilimo na usindikaji wa mazao, anga na usafiri, ufundi mitambo, usafirishaji huduma za majumbani pamoja na fani nyingine nyingi, hivyo amesema Watanzania wanatambulika kwa bidii, unyenyekevu, maadili mema ya kazi na mtazamo chanya kazini.

Kadhalika, Waziri Sangu amemwalika Waziri wa Kazi, Ajira na Ustawi wa Jamii wa Serbia, Mhe. Milica Djurdjevic Stamenkovski kutembelea Tanzania ili kujionea mikakati inayotekelezwa na Serikali katika kuimarisha soko la ajira pamoja na sera za ajira. Pia, amemkaribisha kutembelea vivutio vya utalii nchi ya Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Kazi, Ajira na Ustawi wa Jamii wa Serbia, Mhe. Milica Djurdjevic Stamenkovski, amesema nchi ya Serbia ipo katika mchakato wa kufungua ubalozi nchini Tanzania ili kuendelea kukuza ushirikiano kati ya mataifa hayo. Pia alimwalika Waziri Sangu kutembelea nchi ya Serbia ili kujadili kuhusu masuala ya kazi na ajira ikiwemo fursa za ajira zilizopo nchini humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu akizungumza na Waziri wa Kazi, Ajira na Ustawi wa Jamii wa Serbia, Mhe. Milica Djurdjevic, walipo kutana katika kikao cha pembeni (side meeting) kujadili ushirikiano wa masuala ya Kazi na Ajira, Jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Tanzania wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu alipokutana na kuzungumza na Waziri wa Kazi, Ajira na Ustawi wa Jamii wa Serbia, Mhe. Milica Djurdjevic, katika kikao cha pembeni (side meeting) kujadili ushirikiano wa masuala ya Kazi na Ajira, Jijini Riyadh, Saudi Arabia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com