Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kutoa fursa kwa wazee, katika maana pana ya watu wenye hekima na busara, kujadili na kutoa maoni yao kuhusu misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ili kuendelea kudumisha Tanzania kuwa nchi ya amani, umoja na mshikamano.
Butiku amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuwaleta pamoja wazee na wadau mbalimbali wa jamii ili kujadili na kushauri juu ya namna ya kuimarisha misingi ya amani, umoja na mshikamano wa kitaifa kwa matumaini ya maendeleo endelevu kwa wananchi.
“Lengo kubwa la mkutano huu ni kuwaleta pamoja wazee, katika maana pana ya watu wenye hekima na busara, kujadili na kutoa maoni yao kuhusu misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa ili Taifa letu liendelee kuwa nchi ya amani, umoja na mshikamano kwa matumaini na maendeleo endelevu kwa watu wake,” alisema Butiku.
Ameeleza kuwa mkutano huo utawakutanisha wadau kutoka makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwemo viongozi wa dini, wasomi, wazee wastaafu, wanawake, vijana, vyama vya siasa, wadau wa tasnia ya habari pamoja na taasisi za kiraia.
Kwa mujibu wa Butiku, washiriki wa mkutano huo pia watapata fursa ya kujadili umuhimu wa mazungumzo ya kitaifa katika kuimarisha amani, umoja na maendeleo ya Taifa, hususan katika kipindi hiki kinachofuatia matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Ameongeza kuwa wazee watatoa maoni na ushauri juu ya masuala mbalimbali ya kijamii na kisiasa, hasa yanayohusiana na matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani, kwa lengo la kujenga mustakabali wa Taifa lenye mshikamano, amani na maendeleo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Social Plugin