Na Mwandishi wetu,Dar
Nchi nne zinazopakana na Ziwa Tanganyika zimetakiwa kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za kiusalama, mazingira na uhalifu wa kuvuka mipaka unaotendeka katika ziwa hilo ambalo ni muhimu kwa uchumi wa nchi zinazopakana nalo.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ally Senga Gugu, wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Ushirikiano wa Usalama wa Ziwa Tanganyika wenye lengo la kujadili vitendo vya uharamia na uvuvi haramu Ziwa Tanganyika, leo Januari 19, 2026 Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Gugu alisema mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika katika kukabiliana na uhalifu wa kuvuka mipaka unaofanyika ndani na kandokando ya Ziwa hilo ambapo amesisitiza ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia, utekelezaji wa doria za pamoja na uimarishaji wa uwezo wa vyombo vya utekelezaji wa sheria. Pia, alisisitiza kuendelea kuelimisha wananchi wanaozunguka Ziwa Tanganyika kupitia Polisi Jamii ili kuzuia uhalifu badala ya kusubiri kupambana na uhalifu.
Aliongeza kuwa licha ya umuhimu wa ziwa Tanganyika katika kukuza uchumi wa nchi zinazolizunguka, bado ziwa hilo linaendelea kukabiliwa na vitendo vya uhalifu kama vile uvuvi haramu, magendo ya bidhaa, biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, uhalifu wa mazingira na unyanganyi wa kutumia silaha, hivyo alitoa wito kwa nchi shiriki kuweka mikakati ya pamoja na mshikamano ili kukabiliana nayo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Intelijensia ya Jinai (CP) Charles Mkumbo akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini alisema kuwa, mkutano huo wa pili wa Kimataifa unahusisha pia Wakuu wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tanzania na Zambia.
Aliongeza kuwa uwepo wa Wakuu hao wa Polisi unaonesha dhamira ya pamoja ya nchi hizo katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kuzuia uhalifu unaovuka mipaka na mkutano huo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kujadili mikakati na kutafakari usalama wa Ziwa Tanganyika.
Aidha, alisema mkutano huo unalenga kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyopita, kufuatilia mafanikio yaliyopatikana na kujadili changamoto zilizojitokeza ikiwa ni utekelezaji wa maamuzi ya kikao cha Kamisheni ya pamoja ya kudumu ya ushirikiano wa Ulinzi na Usalama (The Joint Permanent Commission on Defense and Security) (JPDCS) kati ya Tanzania na Zambia pamoja na azimio la Mkutano wa kwanza wa kimataifa uliofanyika mwaka 2023 jijini Dar es Salaam.



Social Plugin