Kanisa la Mlima wa Moto Tanzania limesema linatarajia kufanya maombezi maalum ya kuliombea Taifa la Tanzania kupitia Kongamano la Neno la Mungu lililopewa jina la Anza Mwaka na Bwana.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Kanisa la Mlima wa Moto lililopo Mikocheni B jijini Dar es Salaam, Mchungaji Samwel Hillary, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya kongamano hilo, alisema lengo lao ni kuhakikisha Taifa linaanza mwaka likiwa karibu na Mungu, jambo lililowasukuma kuandaa kongamano hilo.
Mjumbe wa kamati ya Maandalizi ya Kongamano Mchungaji Samwel Hillary akizungumza na Waandishi wa habari katika Kanisa la Mlima wa Moto lililopo Mikocheni B jijini Dar es Salaam.Alisema kongamano hilo litafanyika kuanzia Januari 25 hadi Februari 1, 2026, na linatarajiwa kuongozwa na Askofu Dastani Maboya, Rose Mgeta, Mchungaji Madoshi pamoja na mchungaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa lengo la kuhubiri Neno la Mungu na kuliombea Taifa ili lipate amani ya kweli pamoja na uponyaji katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya kongamano hilo, Godfrey Kazinja, alisema wameamua kuliombea Taifa ili kulinusuru na kulirejesha kwa Mungu, pamoja na kuyahamasisha vizazi na jamii kwa ujumla kuishi katika misingi ya kumpendeza Mungu.
Katibu wa kamati ya Maandalizi ya Kongamano Godfrey Kazinja akizungumza na Waandishi wa habari katika Kanisa la Mlima wa Moto lililopo Mikocheni B jijini Dar es Salaam.
Aidha, Kazinja alisema kutakuwepo na usafiri wa kuwachukua waumini kuanzia eneo la Mwenge hadi kanisani hapo, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata Neno la Mungu na uponyaji.
Naye Sarah Daniel, mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya kongamano hilo, alisema waimbaji mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika tukio hilo, akiwemo John Lissu, Mchungaji Epa, Ashery na wengine wengi, huku akiwaomba Watanzania kuendelea kufuatilia taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Mjumbe wa kamati ya Maandalizi ya Kongamano Sarah Danielakizungumza na Waandishi wa habari katika Kanisa la Mlima wa Moto lililopo Mikocheni B jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za kudumisha amani na upendo miongoni mwa Watanzania, hususan mwanzoni mwa mwaka huu, kwa lengo la kuimarisha mshikamano na maadili ya upendo katika jamii.









Social Plugin