
▪️Lengo ni kurahisisha upatikanaji wa mitaji na mikopo
▪️Mama Lishe Mtumba kugawiwa mashamba kulima mbogamboga
▪️Majiko 1000 yatolewa kwa Mama Lishe
▪️Mtumba wamuunga mkono Rais Samia juu ya matumizi ya Nishati safi
Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Mh. Anthony Mavunde kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx leo amekabidhi jumla ya majiko 1,000 ya gesi kwa mama lishe na baba lishe wa Jimbo la Mtumba, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono jitahada za Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Mavunde amesema mpango huo unalenga kuboresha afya za mama na baba lishe, kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kila siku pamoja na kulinda mazingira kwa kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.
Amesema kuwa Wananchi wa Mtumba kwa kushirikiana Serikali wataendelea kuweka mazingira rafiki kwa wajasiriamali wadogo ikiwemo upatikanaji wa nishati safi kwa makundi mbalimbali ya jamii ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Mavunde pia ameahidi kuanzisha klabu za mama lishe katika kila kata za Jimbo la Mtumba zitakazosaidia kuwaunganisha mama lishe na kuwapatia elimu ya ujasiriamali, uanzishwaji wa miradi ikiwemo mashamb ya kilimo cha Mboga mboga, usimamizi wa fedha pamoja na kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi ili waondokane na mikopo kandamizi maarufu kama kausha damu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mafunzo kutoka kampuni ya Oryx Gas, Peter Ndomba, amewataka mama lishe na baba lishe kuacha kabisa matumizi ya mkaa na kuni akisema nishati hizo zimekuwa zikisababisha madhara makubwa ya kiafya ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa, macho na moyo kutokana na moshi unaotokana na matumizi yake.










Social Plugin