Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC RUVUMA ASHTUKIA ISHU YA USALAMA: AOMBA JUKWAA LA UELEWA KULINDA MIPAKA


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Ahmed Abbas, ametoa ombi rasmi kwa Waziri wa Katiba na Sheria,  Juma Homera, la kuundwa kwa jukwaa la pamoja la uelewa ili kuimarisha ulinzi na usalama wa taifa. 

Ombi hili linakuja kufuatia changamoto za kisheria na kiusalama zinazojitokeza mkoani humo, hususan katika kushughulikia watu wanaoingia nchini kinyume cha sheria.

Mkuu wa Mkoa amebainisha kuwa Ruvuma, ukiwa mkoa wa mipakani, unakabiliwa na wimbi kubwa la raia kutoka nchi jirani wanaoingia kwa njia halali na zisizo sahihi. Changamoto kuu iliyobainishwa ni pamoja na kukamatwa kwa wageni ambao baada ya kufikishwa mahakamani, hupewa hukumu za kifungo cha nje au faini ndogo, hali inayowezesha wao kubaki uraiani badala ya kurudishwa makwao.

Changamoto nyingine ni kuwepo kwa sintofahamu na kutofautiana kwa tafsiri ya kisheria kati ya vyombo vya usalama (vinavyokamata) na mhimili wa mahakama (unaotoa maamuzi).

Mkuu huyo wa mkoa amesema mazingira ya mtuhumiwa kukamatwa leo lakini baada ya siku mbili anaonekana mtaani kunazidi kuleta wasiwasi wa kiusalama kwa wananchi.

Alisema lengo la jukwaa lililoombwa ni kuwakutanisha wataalamu wa sheria, vyombo vya usalama, na wadau wengine ili kujenga uelewa wa pamoja juu ya namna ya kushughulikia mashauri haya bila kuathiri maendeleo ya nchi. Jukwaa hili amesema litasaidia kuondoa sintofahamu katika maamuzi yanayotolewa na mahakama na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unalindwa kwa weledi.

Aidha jukwaa hilo litaimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mahakama, na vyombo vya ulinzi.

Katika hatua nyingine, serikali imeeleza kuendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa mahakama mkoani Ruvuma, ikiwemo Mahakama ya Mwanzo na Mahakama Jumuishi. Ujenzi wa Mahakama Kuu mjini Songea unatajwa kuwa utarahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi kuanzia ngazi za chini, jambo ambalo litaendana sambamba na uimarishaji wa ulinzi wa amani uliosisitizwa na uongozi wa mkoa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com