Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Adolf Ndunguru, amewataka mawakili na wanasheria waliopata mafunzo kuhusu kampeni ya Mama Samia Legal Aid kuzingatia viapo vyao na kutenda haki kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
Ndunguru ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifunga mafunzo ya siku tatu januari 30 ,2026 yaliyowahusisha mawakili na wanasheria kutoka TAMISEMI pamoja na sekretarieti za mikoa, ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa kampeni hiyo katika awamu ya nne.
Amesisitiza umuhimu wa kuepuka vishawishi vya rushwa vinavyoweza kuathiri haki za wananchi, akibainisha kuwa lengo kuu la kampeni hiyo ni kuwarejeshea wananchi tabasamu na imani kwa mfumo wa haki.
“Lengo kuu ni kuwarudishia wananchi tabasamu,” amesema Ndunguru.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, amesema wizara yake imejipanga kikamilifu kukabiliana na migogoro ya ardhi kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid, akieleza kuwa migogoro hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha migongano na kuvuruga amani katika jamii.
Maswi amesema katika awamu za kwanza na za pili za kampeni hiyo, migogoro ya ardhi ilikuwa ikiongoza kwa wingi wa malalamiko yaliyohitaji msaada wa kisheria, ikifuatiwa na migogoro ya mirathi pamoja na changamoto za ndoa.
Tofauti na awamu zilizopita, Maswi amesema awamu ya nne italenga kufuatilia migogoro yote kuanzia mwanzo hadi mwisho ili kuhakikisha inatatuliwa kikamilifu na kuepusha kujirudia kwake.
Aidha, amesema mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika jijini Arusha yamelenga kuwawezesha mawakili na wanasheria wa serikali kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwazi na bila rushwa, ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi wote.
Ili kuimarisha na kuifanya kampeni hiyo kuwa endelevu, Wizara ya Katiba na Sheria imeamua kushirikisha mamlaka za mikoa pamoja na TAMISEMI, kwa kuwa ndizo zilizo karibu zaidi na wananchi katika kutatua changamoto zao za kisheria.
Hata hivyo Maswi ameongeza kuwa hadi kufikia mwezi Juni mwaka 2025, zaidi ya wananchi 4,000 waliwasilisha maombi ya msaada wa kisheria kupitia kampeni hiyo, huku migogoro ya ardhi ikiongoza kwa wingi wa malalamiko.
Amesema hatua inayofuata ni kushirikisha halmashauri zote nchini ili kuongeza wigo wa huduma na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na kampeni hiyo.
“Rais Samia Suluhu Hassan ana nia njema na wananchi wake, ndiyo maana aliipa kampeni hii jina lake. Kufikia Juni mwaka jana, wananchi milioni 4.1 walipata msaada wa kisheria, na tunatarajia kupitia nyinyi, wananchi wengi zaidi watanufaika,” amesema Maswi.



Social Plugin