Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Jeshi la Kujenga Taifa Kikosi cha Mzinga, wameendelea kutekeleza mbinu rafiki za kudhibiti tembo waharibifu bila kuathiri maisha ya watu.
Hatua hiyo inatekelezwa kupitia mafunzo maalum yanayosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika wilaya za Nsimbu na Tanganyika kuanzia Januari 28 hadi 31, 2026.
Katika mafunzo hayo, wananchi wamefundishwa matumizi ya vifaa rafiki ikiwemo mabomu baridi, kifaa cha mpira makelele na kishikio maalum cha kilipuzi kwa ajili ya kufukuza tembo mashambani na maeneo ya makazi kwa usalama.
Aidha, wananchi wameendelea kuelimishwa kuhusu kilimo mbadala kinachostahimili tembo kama pilipili kichaa, ufuta, alizeti, tangawizi, manjano na bamia, pamoja na ufugaji wa nyuki kandokando ya mashamba ili kuongeza ulinzi na kipato.
Mbinu rafiki za kudhibiti tembo bila kuwaua zinaendelea kuleta tija kwa wananchi, huku zikilenga kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha maisha ya jamii.













Social Plugin