
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA- ZNZ), Bi Asha Abdi Makame amempongeza na kumshukuru kwa dhati aliyekuwa Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dkt. Mzuri Issa Ali, kwa uongozi wake uliotukuka na mchango wake mkubwa wa kuimarisha taasisi hiyo katika kipindi chote cha uongozi wake.
Amesema juhudi, maono na uadilifu wa Dkt. Mzuri vimeweka misingi imara ya mafanikio ya TAMWA- ZNZ katika kutetea haki za wanawake na watoto pamoja na kupaza sauti za wanawake kupitia vyombo vya habari.
Bi Asha ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TAMWA -ZNZ zilizopo Tunguu, katika hafla ya kumuaga Dkt Mzuri Issa na kumkaribisha Mkurugenzi mpya Bi Nairat Abdulla Ali.
Akieleza kuhusu mchakato wa kupatikana kwa Mkurugenzi mpya, Bi Asha alisema kuwa TAMWA- ZNZ ilifuata kwa makini Sera ya kurithishana madaraka, ambayo ni utaratibu maalum unaotumika katika taasisi za umma na binafsi ili kuhakikisha kuwepo kwa viongozi wenye ujuzi, uwezo na maandalizi ya kuchukua madaraka pale kiongozi aliyepo anapostaafu au kuondoka madarakani.
Alisisitiza kuwa Sera hiyo imelenga kulinda uendelevu wa taasisi na kuhakikisha majukumu ya uongozi yanaendelea kutekelezwa kwa ufanisi bila kuathiri mwelekeo na malengo ya TAMWA -ZNZ.
Katika utekelezaji wa Sera hiyo, TAMWA -ZNZ iliunda kamati ya kurithishana madaraka mwaka 2020. Kamati hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi na kujumuisha wajumbe wawili wa Bodi, mwanachama mwandamizi pamoja na Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ.
Kamati hii ilifanya kazi kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 ikisimamia na kuratibu mchakato mzima wa maandalizi na uteuzi ili kuhakikisha upatikanaji wa uongozi madhubuti na endelevu kwa taasisi.
Aidha, Mwenyekiti huyo aliwataka wafanyakazi, wanachama wa TAMWA- ZNZ pamoja na wadau wote kumpa ushirikiano wa dhati Mkurugenzi mpya ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Kwa upande wake Mkurugenzi mpya wa TAMWA -ZNZ, Bi Nairat Abdulla Ali alisema anapokea jukumu hilo kwa unyenyekevu na heshima kubwa, akitambua dhamana nzito aliyopewa na mchango mkubwa ambao TAMWA- ZNZ imekuwa ikiutoa katika jamii.
Alieleza kuwa anaamini kupitia ushirikiano na maono ya pamoja, taasisi hiyo itaendelea kuimarika na kuwa chombo imara cha utetezi wa haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
Bi Nairat alisema uongozi wake utaweka mkazo katika kufanya kazi kwa karibu na waandishi wa habari wa ndani na nje ya Zanzibar, kuimarisha ushirikiano na asasi za kiraia, pamoja na kuendeleza harakati za kuwawezesha wanawake na watu wenye ulemavu kiuchumi.
Aliongeza kuwa TAMWA -ZNZ itaendelea kufanya uchechemuzi wa sheria kandamizi, kupaza sauti za makundi yaliyo pembezoni, na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa haki za binadamu.
Akihitimisha, Bi Nairat aliwaomba wanachama wa TAMWA -ZNZ, waandishi wa habari, washirika wa maendeleo na wadau wote kuendelea kutoa ushirikiano katika safari ya kuijenga taasisi hiyo.
Aliahidi uongozi unaosikiliza, unaochukua hatua kwa wakati na unaotanguliza matokeo, akisisitiza kuwa jukumu la sasa si kuanza upya bali kujenga juu ya misingi imara iliyoachwa na Dkt. Mzuri Issa Ali ili kuhakikisha TAMWA Zanzibar inaendelea kukua na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano
TAMWA ZNZ








Social Plugin