Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MIKATABA YA SH TRILIONI 1.2 YASAINIWA KUSAMBAZA UMEME VITONGOJI 9,009



Na Mwandishi wetu,Dodoma

Serikali imesaini mikataba yenye thamani ya shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kusambaza umeme katika vitongoji 9,009 nchini, hatua inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kuanzia ngazi ya chini .
Hafla ya kusaini mikataba hiyo imefanyika jijini Dodoma leo January 17,2026 , ikihusisha zaidi ya wakandarasi 30 , 21 kati yao ni kutoka kampuni za wazawa na tisa Kampuni za kigeni.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alisema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliyeagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha vitongoji vyote 64,359 nchini vinafikiwa na umeme ifikapo mwaka 2030.

Amesema tayari vijiji vyote nchini vimefikiwa na umeme na sasa nguvu kubwa inaelekezwa katika vitongoji ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma katika maendeleo ya nishati.

Waziri Ndejembi amesisitiza kuwa hakuna uchumi wa kisasa unaoweza kukua bila nishati ya uhakika, akieleza kuwa mradi huo utaanza kwa kuunganisha zaidi ya wananchi laki mbili na utaongeza thamani ya shughuli za uzalishaji, biashara na huduma za kijamii.

Ametaja mikoa ya Kilimanjaro, Kigoma na Katavi kuwa miongoni mwa itakayonufaika kwa kiwango kikubwa zaidi baada ya mradi kukamilika, huku akiongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na benki na taasisi za kimataifa kufanikisha upatikanaji wa umeme nchi nzima.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, amesema mradi huo ni mapinduzi makubwa ya maendeleo kwani Serikali sasa imeanza kuhesabu vitongoji vinavyohitaji umeme badala ya mikoa.

Amesema kile kinachoonekana mijini sasa kitaonekana pia kwenye vitongoji na kubainisha kuwa watoto waliokuwa wakisoma kwa mwanga wa kibatari sasa watanufaika na mazingira bora ya kujifunzia kupitia umeme wa uhakika.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Hassan Said, amesema mradi umeandaliwa kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia hali halisi ya upatikanaji wa umeme kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa REA haitavumilia ukiukwaji wa maadili, rushwa au udanganyifu kwa wananchi, akieleza kuwa mchango wa kuunganisha umeme ni shilingi 27,000 .

Ameonya kuwa mkandarasi yeyote atakayekiuka mkataba au kuwarubuni wananchi atalazimika kuvunjiwa mkataba mara moja.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Lazaro Twage, Mhandisi Frank Chambua alisema TANESCO ndiyo mshauri elekezi wa mradi huo na itashirikiana kwa karibu na REA kuhakikisha gharama za kuunganisha umeme zinazingatia mahitaji ya mwananchi mmoja mmoja.

Ameeleza kuwa mwananchi anaweza kuunganishiwa umeme hata kwa chumba kimoja kulingana na uwezo na matumizi yake.

Ameongeza kuwa TANESCO imeanza kubadilisha nguzo za miti kuwa nguzo za zege kutokana na changamoto ya kuoza kwa nguzo za zamani, hatua itakayopunguza gharama za matengenezo kwa muda mrefu, huku akisisitiza ushirikiano wa wananchi katika kulinda miundombinu hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema umeme ni kichocheo kikuu cha mabadiliko ya uchumi wa wananchi, akieleza kuwa utaongeza thamani ya shughuli za uzalishaji, viwanda vidogo, biashara na huduma za kijamii kama afya na elimu.

Amebainisha kuwa Mkoa wa Dodoma una kata 209 na vijiji 564 ambavyo vyote tayari vimefikiwa na umeme, huku vitongoji 1,770 kati ya 3,214 vikiwa tayari na huduma hiyo, akieleza kuwa mradi huu utakamilisha wigo wa umeme katika vitongoji vilivyosalia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, aliipongeza serikali kwa kuendelea kuwekeza katika nishati vijijini, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Amewataka wakandarasi kutekeleza miradi hiyo kwa weledi, kuzingatia thamani ya fedha na muda wa kazi, huku akibainisha kuwa kamati itafanya ziara za ufuatiliaji kuhakikisha uwajibikaji unazingatiwa.

Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi, Mhandisi Maulid Seif alisema wanashukuru serikali kwa kuendelea kutoa fursa kwa wazawa kushiriki katika miradi mikubwa ya kitaifa.

Ameeleza kuwa matarajio ya baadaye ni kuona miradi mikubwa ikitekelezwa na wakandarasi wazawa pekee ili Watanzania wanufaike zaidi na rasilimali zao, huku akiahidi kuwa miradi hiyo itatekelezwa kwa wakati ili wananchi wapate huduma stahiki.

Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuchukua muda wa miaka mitatu, ambapo miezi ya awali itaelekezwa katika maandalizi ya kitaalamu na upangaji wa miundombinu, hatua inayotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi katika vitongoji nchini.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com