Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza kuidhinisha mifumo 10 ya tiketi mtandao baada ya kampuni hizo kukidhi matakwa ya kisheria, huku ikieleza kuwa mifumo mingine imeshindwa kufikia viwango vilivyowekwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano cha LATRA, Salum Pazy, amesema idadi ya mifumo iliyoidhinishwa imeongezeka kutoka mitano iliyokuwepo mwishoni mwa mwaka 2025 hadi kufikia 10 kufikia Januari 2026.
Amesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto kwa baadhi ya watoa huduma waliochelewa kukamilisha taratibu za kisheria, hali iliyosababisha mifumo yao kusitishwa kwa muda hadi watakapokidhi vigezo vinavyotakiwa.
LATRA imewataka wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani kuacha mara moja kutumia mifumo isiyoidhinishwa, huku ikitoa siku 14 kuanzia sasa kwa wasafirishaji kuhamia kwenye mifumo halali.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa baada ya Februari 15, 2026, mabasi yatakayobainika kutumia tiketi mtandao isiyoidhinishwa hayataruhusiwa kutoa huduma, sambamba na kunyimwa leseni au kushindwa kuhuishwa kwa leseni zao.
Kwa upande wa abiria, LATRA imewasisitiza kununua tiketi mtandao kupitia mifumo rasmi na kutumia programu ya LATRA App kuhakiki tiketi na nauli, huku ikiwahimiza kutoa taarifa za ukiukwaji ili kuboresha usafiri wa umma nchini.








Social Plugin