Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AMANI NI AJENDA ISIYO NA MBADALA: WABUNGE NA WANANCHI WASISITIZA UTULIVU KUCHOCHEA MAENDELEO



Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamesisitiza kuwa amani ni ajenda isiyo na mbadala na ni lazima ilindwe kwa wivu ili mipango mikubwa ya maendeleo inayopangwa na serikali iweze kutekelezeka kwa ufanisi.

Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma wakati wabunge hao wakijadili hotuba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Novemba 14, 2025 wakati akifungua Bunge la 13 ambapo imetajwa kuwa dira ya kuelekea maendeleo ya kweli kwa wananchi.

Mbunge wa Kisarawe Dk Selemani Jafo ameeleza kuwa ajenda ya amani haina mbadala na amewaomba Watanzania wote kuilinda kwa nguvu zote kwani mipango ya maendeleo haitakamilika iwapo amani itavurugika.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete aliyesema kuwa ili kuenzi kazi kubwa na nzuri zinazotambulika ndani na nje ya nchi zinazofanywa na Rais Samia ni vyema Watanzania wakaendelea kutunza na kuilinda amani kwa sababu ndiyo kila kitu katika maendeleo ya taifa lolote duniani.

Naye Mbunge wa Kalenga Jackson Kiswaga amesisitiza kuwa wabunge na wananchi wana wajibu wa kuliombea taifa amani ili utekelezaji wa mipango ya serikali utimie akitolea mfano wa namna ahadi za ajira zilivyoanza kutekelezwa ambapo katika jimbo lake wamepata watumishi wapya 194.

Aidha Mbunge wa Viti Maalumu Kijakazi Yunus amebainisha kuwa upendo na uwajibikaji wa Rais umesaidia kupunguza changamoto za wananchi ikiwemo kuongezeka kwa upatikanaji wa maji mkoani Lindi kutoka asilimia 58 hadi 75 hali inayoinua ustawi wa wanawake na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wao wananchi kutoka maeneo mbalimbali wameelezea kiu yao ya kuona utulivu unadumu baada ya kipindi cha uchaguzi ili kuleta mshikamano wa kitaifa na kuponya tofauti za kisiasa.

Happiness Mkubilu ambaye ni mkazi wa Tunduma amesema amani baada ya uchaguzi hujenga mazingira bora ya serikali kuwajibika kwa ahadi ilizozitoa wakati wa kampeni na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora. Jerse Mwang’onda mkazi wa Songwe amesisitiza kuwa bila amani hakuna maendeleo na demokrasia haiwezi kukua ipasavyo bila ushiriki wa amani katika michakato ya kisiasa.

Tahadhari zaidi imetolewa na Thokozan Mwangosi mkazi wa Ileje ambaye amewataka Watanzania kuepuka migogoro isiyo ya lazima kuanzia ngazi ya familia hadi taifa ili kuzuia nchi kuingia katika machafuko yanayoweza kuwafanya wananchi wawe wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe.

Viongozi na wananchi wanakubaliana kuwa hotuba ya Rais imetoa dira ya wapi taifa linaelekea na sasa nguvu zote zinapaswa kuelekezwa katika kudumisha utulivu ili rasilimali za taifa kama dhahabu zitumike kwa maslahi ya miradi ya kimkakati bila kuyumbishwa na maoni ya wakosoaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com