Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHENGERWA ATEMBELEA KITUO CHA AFYA KALOLENI 'SITARAJII WAGONJWA KUNUNUA DAWA NJE YA KITUO'


Na Bora Mustafa,Arusha.

Waziri wa Afya, Mhe. Mchengerwa, amefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Afya Kaloleni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kufuatilia utoaji wa huduma za afya kwa wananchi. Ziara hiyo imelenga kukagua hali ya huduma, upatikanaji wa dawa pamoja na utendaji wa watumishi wa afya katika kituo hicho.

Katika ziara yake, aliyoifanya Januari 26,2026 Waziri wa Afya Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa sekta ya afya inapaswa kupewa kipaumbele cha juu, pamoja na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinashughulikiwa kwa wakati. 

Amesema kutakuwa na namba maalum zitakazotumika kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za afya, hata hivyo ameeleza kuwa watoa huduma watakaokiuka maadili au kutoa huduma duni watachukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa hatarajii kuona wagonjwa wakinunua dawa nje ya vituo vya afya.

 Pia ameeleza kuwa kuna baadhi ya madaktari wenye maduka binafsi ya dawa (pharmacy) wanaowaelekeza wagonjwa kwenda kununua dawa nje, jambo alilolionya vikali na kuagiza hatua zichukuliwe mara moja dhidi ya wahusika.

Hata hivyo, Mhe. Mchengerwa amempongeza mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Kaloleni kwa kazi nzuri, akisema ameridhishwa na hali ya kituo hicho kwani kina vifaa tiba vya kutosha. Amesema kituo hicho kina kila sababu ya kupandishwa hadhi na kuwa hospitali ya kisasa ya wilaya.

Na pia Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa msongamano wa wagonjwa katika kituo hicho unaashiria kuwepo kwa huduma bora zinazowavutia wananchi wengi kufuata matibabu hapo.

Aidha, amemuagiza  Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kumpatia cheti cha pongezi mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Kaloleni kwa utendaji wake mzuri.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya, Mhe. Joseph Mkude, amesema kuwa tiba ni utalii na utalii ni tiba, akieleza kuwa huduma bora za afya ni sehemu muhimu katika maandalizi ya michuano ya AFCON.


Pia, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Ndugu John Kayombo, ametoa pongezi kwa uongozi wa mkoa, wilaya pamoja na uongozi mzima wa Kituo cha Afya Kaloleni. Amesema kuna baadhi ya vifaa tiba vilivyopo kituoni hapo ambavyo hata hospitali za mkoa hazina vifaa hivyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com