Diwani wa Kata ya Mjini Mathew Ngalimanayo(alieshika jembe) akiwa anafanya usafi na baadhi ya viongozi wa kata ya mjini katika kuelekea kuadhimisha miaka 49 ya Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanayofanyika kila mwaka tarehe 5 Februari, Diwani wa Kata ya Mjini, Mathew Ngalimanayo, ameongoza zoezi la usafi wa mazingira pamoja na viongozi na wanachama wa CCM Kata ya Mjini, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Zoezi hilo limefanyika leo Januari 26, 2026, likihusisha matawi manne ya kata hiyo, sambamba na kuwatazama na kuwapa heshima waasisi wa chama waliopo katika manispaa hiyo.
Akizungumza na baadhi ya viongozi wa ngazi ya tawi katani humo Ngalimanayo amesema CCM ina wajibu wa kuwatumikia wananchi kwa vitendo, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na mshikamano kwa kila mwananchi.
Amesema chama kitaendelea kusikiliza kero na changamoto za wananchi ili “kutibu vidonda” vinavyosababisha malalamiko, na kuwataka viongozi kuwa mabalozi wa amani kwa kutoa elimu ya kuhamasisha utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Aidha, Diwani huyo amewashukuru wanachama na viongozi wa kata kwa ushirikiano wao, na kuwasisitiza kuyatekeleza kwa vitendo yale yote yaliyozungumzwa.
Amesema mshikamano uliopo ni msingi muhimu wa kuimarisha chama na kuendelea kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, katibu wa tawi la Mjini, Bi. Marry Haule, amesema kuelekea siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa CCM, wanachama wameamua kuonesha mfano kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya tawi hilo.
Ameongeza kuwa watakuwa mabalozi wazuri wa amani na utulivu, akisisitiza kuwa CCM iko kazini na wanachama hawapaswi kuogopa kuonesha uanachama wao.
Ikumbukwe kuwa kila mwaka ifikapo tarehe 5 Februari, CCM huadhimisha kumbukizi ya kuanzishwa kwake, ikiwa ni fursa ya kutafakari na kuimarisha mshikamano wa chama.


Social Plugin