Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JESHI LA KUJENGA TAIFA LAFUNGUA FURSA YA MAFUNZO KWA VIJANA KWA MWAKA 2026





Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza kuanza kwa mafunzo ya kujitolea kwa vijana wa Tanzania Bara na Visiwani kwa mwaka 2026, yakilenga vijana wenye umri wa miaka 16 hadi 18 waliomaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali.

Akizungumza Januari 20, 2026 jijini Dodoma, Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, amesema mafunzo hayo hayalengi kutoa ajira bali kuwajenga vijana kiakili, kimwili na kimaadili ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha na kuchangia maendeleo ya taifa.

Amesema washiriki watanufaika kwa kupata elimu ya uzalendo, nidhamu ya kazi, stadi za maisha na mafunzo ya vitendo yatakayowawezesha kujitegemea baada ya kuhitimu.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena, waombaji wanapaswa kuwa raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 16 hadi 18, waliomaliza elimu ya darasa la saba kwa Tanzania Bara au kidato cha pili kwa Zanzibar kati ya mwaka 2022 hadi 2025, wakiwa na vyeti halisi vya kuhitimu.

Ameongeza kuwa JKT linawahimiza pia vijana wenye taaluma mbalimbali hususan za teknolojia ya habari na mawasiliano kujitokeza kuomba nafasi hizo, ikiwemo fani za IT, ICT, Cyber Security na taaluma nyingine zinazohusiana na kompyuta.

Usajili wa mafunzo hayo utaanza rasmi tarehe 26 Januari 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, huku vijana watakaoteuliwa wakitakiwa kuripoti kwenye makambi ya JKT kuanzia tarehe 27 Februari hadi 4 Machi 2026.

Aidha, JKT limekumbusha kuwa halitoi ajira bali hutoa mafunzo yanayowawezesha vijana kujiajiri na kujitegemea. Maelezo zaidi kuhusu sifa na vifaa vinavyohitajika yanapatikana kupitia tovuti ya JKT www.jkt.mil.tz.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com