Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT JUMA ZUBERI HOMERA AANZA ZIARA YA SIKU TATU AANGAZIA UJENZI WA MAHAKAMA NA MABORESHO YA HAKI

Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Zuberi Homera akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed alipowasili Ofisini hapo kabla ya kuanza ziara yake Jimboni kwake Namtumbo 

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Dkt Juma Zuberi Homera, amewasili leo Januari 16, 2026 katika Jimbo la Namtumbo kwa ziara ya siku tatu yenye lengo kuu la kuwashukuru wananchi kwa imani kubwa waliyoionesha kwake kwa kumchagua na kumpigia kura za kutosha. 

Katika ziara hiyo, Dkt Homera ametembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa huo, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, kuhusu masuala mbalimbali ya katiba, sheria na maendeleo ya miundombinu ya utoaji wa haki.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt Homera ameeleza kuwa ujenzi wa majengo ya taasisi za haki ni miongoni mwa mafanikio makubwa yanayoendelea nchini, akitolea mfano jengo la Likuyusekamaganga wilayani Namtumbo pamoja na jengo la Mahakama Jumuishi la Msamala. 

Amesema jengo hilo litahudumia kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama Kuu, na litawasaidia wananchi kupata haki kwa urahisi ikiwemo masuala ya ndoa, mirathi, usuluhishi na mashauriano ya kisheria.

 Ameeleza kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, na itaenea katika mikoa mingine sambamba na ujenzi wa majengo ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Dkt Homera pia amegusia mradi wa Nalasi unaohusisha ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo, akieleza kuwa imani yake kuwa kuboreshwa kwa miundombinu hiyo kutaimarisha mazingira ya utoaji wa haki nchini. 

Aidha, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Ruvuma kuendelea kulinda amani, huku akibainisha kuwa wizara yake inaendelea na maandalizi ya marekebisho ya sheria za haki za jinai, ikiwemo kuboresha taratibu za uchunguzi kabla ya kufungua mashitaka na masuala ya ukamataji. 

Ameongeza kuwa wizara itafanya ziara rasmi ya kukagua miradi yote ya sekta ya sheria na pia kuendesha kampeni ya Samia Legal Aid kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuupa mkoa huo mawaziri wawili akiwemo Dkt Juma Homera na Mheshimiwa Judith Kapinga. 

Amesema mkoa wa Ruvuma ni mkoa ambao upo mpakani na unakumbana na changamoto za wahamiaji haramu na utekelezaji wa adhabu za kisheria, hususani  kifungo cha nje kwa raia wasiokuwa watanzania. 

Ameomba kuwepo kwa majukwaa ya kisheria yatakayokutanisha wataalamu wa sheria na vyombo vya ulinzi ili kupata uelewa wa pamoja, pamoja na kushughulikia changamoto ya ardhi. 

Amesema  kuwa mkoa uko tayari kushirikiana kikamilifu na wizara ya Katiba na Sheria katika kulinda amani na kuimarisha haki bila migongano ya kiutendaji.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com