Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AFUA ZA LISHE ZAZAA MATUNDA SHINYANGA, RC MHITA ASISISTIZA UWAJIBIKAJI NA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akifungua kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka 2024/2025 pamoja na utoaji wa elimu ya Bima ya Afya kwa Wote, kilichofanyika Januari 16, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa Shinyanga.

Na Sumai Salum-Shinyanga

Mkoa wa Shinyanga umefanya kikao kazi maalum cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe pamoja na bima ya afya kwa wote, kikilenga kuimarisha ustawi wa afya za wananchi hususan watoto na makundi yaliyo hatarini.

Kikao hicho kimefanyika Januari 16, 2026 katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, kikihusisha viongozi wa mkoa, wilaya, halmashauri pamoja na wadau wa sekta ya afya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti katika utekelezaji wa afua za lishe, akieleza kuwa lishe bora ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Mhe. Mhita amewapongeza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Madiwani kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa afua za lishe na afya kwa ujumla, akibainisha kuwa jitihada zao zimeanza kuzaa matunda kupitia mafanikio yanayoonekana katika viashiria mbalimbali vya lishe mkoani humo.

Ametaja takwimu zinazoonesha mafanikio hayo, akieleza kuwa kiwango cha udumavu kwa watoto kimepungua kutoka asilimia 32.1 hadi asilimia 27.5, kiwango cha ukondefu kwa watoto kimeshuka kutoka asilimia 4.3 hadi asilimia 1.3, huku uzito pungufu kwa watoto ukipungua kutoka asilimia 13.3 hadi asilimia 8.6.

Pamoja na pongezi hizo, Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi hao kusimamia kwa mkazo zaidi utekelezaji wa afua za lishe na afya kwa kuzingatia mkataba uliopo, uwajibikaji, ufuatiliaji wa karibu na matumizi sahihi ya rasilimali zilizotengwa kwa ajili ya kuboresha afya za wananchi.

Akizungumza pia kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote, Mhe. Mhita amesema kuwa kujiunga na bima ya afya kutawapunguzia wananchi gharama za matibabu, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima kati ya wananchi na watumishi wa sekta ya afya.

“Nitumie fursa hii kuwashukuru sana Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Madiwani kwa kusimamia utekelezaji wa afua hizi za afya. Pia nisiwasahau wadau wetu mbalimbali wakiwemo wazazi, vikundi vya kijamii, taasisi binafsi pamoja na waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika kuelimisha jamii. Aidha, bima ya afya itawapunguzia gharama wananchi na kusaidia kuondoa malalamiko kwa watumishi wa afya kwa kuwa huduma zitapatikana kwa utaratibu unaoeleweka,” ameongeza Mhe. Mhita.

Katika kikao hicho, washiriki wamepata elimu kuhusu bima ya afya kwa wote kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), ambapo walielimishwa umuhimu wa wananchi kujiunga na bima ya afya ili kupata huduma bora, endelevu na kwa gharama nafuu.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, amewataka washiriki kutumia elimu waliyoipata kama chachu ya kuimarisha afya za watoto na jamii kwa ujumla, akisisitiza kuwa maarifa hayo yanapaswa kuonekana katika utekelezaji wa vitendo ngazi ya jamii.

Mhe. Masindi amehitimisha kwa kutoa wito kwa wadau wote wa afya kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kutathmini utekelezaji uliopita, kubaini changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utekelezaji wa afua za lishe na kufanikisha lengo la bima ya afya kwa wote kwa manufaa mapana ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, akizungumza wakati akifunga kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka 2024/2025 na elimu ya Bima ya Afya kwa Wote, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, Januari 16, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa, Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mhe. Franc Nkinda, akifuatilia kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka 2024/2025 na elimu ya Bima ya Afya kwa Wote, kilichofanyika Januari 16, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa, Shinyanga.
Afisa lishe Mkoa wa Shinyanga Mussa Makungu akielezea matokeo ya utekelezaji mkataba wa lishe kipindi cha Julai-Disemba 2025














































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com