Na Sheila Ahmadi – Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuimarisha sekta ya uchukuzi nchini kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kimataifa, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050.
Akizungumza leo Januari 16,2026 jijini Dar es Salaam mara baada ya uzinduzi wa Jengo la Viongozi Mashuhuri (VIP Lounge) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu na huduma za usafiri kupitia viwanja vya ndege, usafiri wa anga, reli na bandari.
Amesema kuwa kuimarishwa kwa Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuunganisha Tanzania na mataifa mengine, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ushindani wa kiuchumi.
Dkt. Nchimbi amefafanua kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya uchukuzi kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ikiwemo ujenzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) unaopita eneo la Posta hadi Gongolamboto, ambao utaunganishwa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ili kurahisisha usafiri wa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
“Kupitia sekta ya uchukuzi, Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kwa vipande mbalimbali, ikiwemo maeneo ambayo hayakuwa yamekamilika kama Tabora, Mwanza, Kigoma hadi Msongati nchini Burundi. Sambamba na hilo, kuna uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na bandari nyingine za kimkakati ikiwemo Tanga, Mtwara, Kisiwa Mgao, Mbamba Bay, Kigoma na Bagamoyo,” amesema Dkt. Nchimbi.
Ameongeza kuwa Serikali pia inaendelea na uboreshaji wa Reli ya TAZARA pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara za kiwango cha lami zinazounganisha Tanzania na nchi jirani, hatua inayochangia kukuza biashara ya kikanda.
Dkt. Nchimbi amesema mafanikio ya sekta ya uchukuzi yamechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa, ambapo Pato la Taifa limeongezeka kutoka asilimia 7.2 mwaka 2023 hadi asilimia 7.5 mwaka 2024. Aidha, ukuaji wa sekta ya uchukuzi umeongezeka kutoka asilimia 4.1 mwaka 2023 hadi asilimia 4.2 mwaka 2024, huku wastani wa hivi karibuni ukiwa asilimia 5.4.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Wizara inaendelea kuhakikisha miradi yote ya viwanja vya ndege nchini inaboreshwa ili kuendana na ongezeko la huduma za usafiri wa anga, hatua inayofungua fursa mbalimbali za kiuchumi.
Profesa Mbarawa ameongeza kuwa kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, sekta ya anga ina mchango mkubwa katika kuimarisha utalii, kilimo na biashara. Amesema upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unaendelea kufanyika kwa viwanja vipya vya ndege ikiwemo Serengeti, Kagera, Njombe, Iringa na Tanga.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo, amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi unaolenga kuimarisha miundombinu na huduma za viwanja vya ndege nchini.



















Social Plugin