Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM YAJIKITA KUSHUGHULIKIA KERO ZA WANANCHI NA KUFUATILIA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA SERIKALI




Na Mwandishi wetu,DODOMA

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza maandalizi ya ziara ya kitaifa ya kusikiliza kero za wananchi na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Serikali, huku akihamasishwa mshikamano kati ya chama na wananchi katika kuhakikisha maendeleo yanatimizwa.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenan Kihongosi, amesema jana Jijini Dodoma kuwa ziara hiyo itaanzia mkoani Singida, na inalenga kutoa nafasi kwa wananchi kueleza changamoto zao, pamoja na kuhakikisha ahadi zote za Serikali zinafikiwa kwa vitendo.

“Kama chama tuliahidi kufuatilia utekelezaji wa miradi na ahadi za Serikali. Ziara hii ni jukwaa la kuwasikiliza wananchi na kutatua changamoto zao, ili tuhakikishe kila ahadi inatimizwa kwa manufaa yao,” alisema Kihongosi.

Aidha, Kihongosi alionya dhidi ya kueneza habari zisizo sahihi zinazotaka kuharibu imani ya wananchi kwa Serikali, akisisitiza kuwa historia na ukweli havitaruhusiwi kuchafuliwa kwa maslahi ya watu binafsi. “Siasa za kitaifa zinapaswa kuendeshwa kwa hoja na si jazba. Vyama vyote vya siasa vinaalikwa kushiriki katika mijadala ya kujenga,” aliongeza.

Katibu huyo alitoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyolinda hadhi ya Tanzania kimataifa, akirejelea mkutano wake na mabalozi Januari 15, 2026, ambapo hatua hiyo imeimarisha diplomasia ya nchi na kuonyesha mwelekeo chanya wa uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa.

Aidha, Kihongosi alisisitiza mafanikio ya Serikali katika ukusanyaji wa kodi, akisema makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yamefikia Sh trilioni 3.1, huku Desemba yakivuka Sh trilioni 4, jambo ambalo linaonyesha ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini.

Akizungumzia wastaafu, Kihongosi alisema CCM inawaheshimu viongozi waliotumikia Taifa, lakini aliwataka kufurahia maisha ya kustaafu bila kutoa malalamiko, huku wakiendelea kuwa mashauri wazuri kwa viongozi waliopo.

Kuhusu bima ya afya kwa wote, Kihongosi alisema Serikali inachukua hatua madhubuti za kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa kila Mtanzania, ikiwemo kuondoa tabia ya kuzuia maiti kwa wagonjwa wasiolipa gharama za matibabu.

Aidha, alibainisha kwamba Serikali imetoa ajira zaidi ya 12,000 nchini na mpango wa kutoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya vijana bado unaendelea kufanyiwa maandalizi, kwa lengo la kuongeza fursa za ajira na kukuza maendeleo ya kiuchumi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com