Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU MGENI RASMI BUNGE BONANZA


Na Josephine Manase, Dodoma

Dodoma. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Bunge Bonanza litakalofanyika jumamosi 31 Januari 2026 kwenye viwanja vya shule ya sekondari John Merlin Miyuji, Dodoma.

Tukio hilo linatarajiwa kuwa jukwaa la mshikamano na burudani, likihusisha mashabiki wa timu za soka za Simba na Yanga, pamoja na washiriki kutoka vyuo mbalimbali, Wizara za Kilimo, Ulinzi na Vijana, ambao wataungana kushiriki michezo na burudani .

Mwenyekiti wa Bunge Bonanza Festo Sanga, ameeleza kuwa moja ya vipengele vya kipekee vya bonanza hili ni washiriki kujitoa kuchangia damu salama kwa hiari.

Amesema shughuli hiyo inalenga kuokoa maisha ya wagonjwa, kuondoa dharura za kiafya, na kuimarisha mshikamano wa kijamii kati ya washiriki na jamii kwa ujumla.

Amesema kuchangia damu ni kitendo cha huruma kinachoongeza uelewa wa kijamii kuhusu umuhimu wa afya na mshikamano wa kitaifa.

"Bunge Bonanza linahusisha mashindano ya michezo ya burudani, ikiwemo mpira wa miguu, kuruka kamba, pete, mashindano ya kula, kufukuza kuku, pamoja na michezo mingine yenye lengo la burudani na mshikamano, " amesema.

Ameeleza Washiriki wote, wakiwemo wabunge na watumishi wa bunge, wataanza matembezi ya pamoja kuanzia saa 12 kamili asubuhi jirani na Chuo cha Mipango Dodoma kabla ya kuanza kwa michezo rasmi.

Amefafanua kuwa shughuli za michezo na burudani zinaunganishwa na zawadi maalumu kwa washiriki watakaoshinda jambo linalosaidia kukuza mshikamano.

Bunge Bonanza linahamasisha ushirikiano kati ya mashabiki, wabunge, watumishi wa bunge, na wadau wa jamii, huku likilenga kuboresha malezi kwa vijana, afya ya jamii, na mshikamano wa kijamii.

Meneja Mahusiano wa Azania benki Elizabeth Nyayega amesema benki hiyo imekuwa ikisaidia bonanza vifaa vya michezo na huduma nyingine za kimfumo, huku ikidhamiria kutoa huduma za kibenki kwa washiriki na jamii.

Amesema ushiriki wa Azania Benki kama mdhamini Mkuu wa bonanza hilo umeimarishwa huku akitaja faida za michezo kuwa ni kuboresha afya, mshikamano wa kijamii, malezi kwa vijana, na maendeleo endelevu ya jamii.

Mmoja wa mashabiki wa timu ya Simba Julian Hamoga ameshauri utoaji wa nishani unapaswa kufanyika kwa utaratibu mzuri tofauti na Miami mingine kuhakikisha burudani inaendelea kwa mpangilio bora .

Bunge Bonanza limeendelea kuwa jukwaa la mshikamano wa kijamii, burudani, na malezi, likiimarisha mshikamano wa kitaifa kati ya mashabiki, wabunge, watumishi wa bunge, na wadau wa jamii, huku likichangia maendeleo endelevu ya michezo na ustawi wa kijamii Dodoma na Tanzania kwa ujumla.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com