Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete
Mkuu wa mkoa wa Pwani Bw. Aboubakar Kunenge
Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU nchini Bw. Crispin Chalamila
***
NA. ELISANTE KINDULU, CHALINZE.
WAZIRI wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Mh. Ridhiwani Kikwete ameisifu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa uadilifu nchini.
Mh. Ridhiwani ameyasema hayo Januari 24, 2026 katika hotuba yake ya kuzindua jengo la ofisi ya TAKUKURU mjini Chalinze.
Mh. Kikwete amesema kati ya fedha zilizotumika, kiasi cha shilingi milioni 8 zilibaki na TAKUKURU wamerejesha fedha hizo Serikalini.
"Kama wewe mkurugenzi wa TAKUKURU na watendaji wako mngekuwa sio wazalendo na waadilifu mngeamua tu ninyi na fundi kupiga dili na hiyo chenji iliyobaki mngeamua kugawana",alisema Mh. Ridhiwani.
Aidha Mh. Waziri ameagiza miradi yote ya ujenzi ndani ya TAKUKURU kutumia mafundi wa ndani kama walivyofanya TAKUKURU Chalinze ili mzunguko wa fedha unufaishe wakazi wa eneo husika.
Akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza, Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU nchini Bw. Crispin Chalamila aliiambia hadhira hiyo kuwa mradi huo wa ofisi ulianza Mwezi Mei 2024 na kukamilika Januari 2025 huku kiasi cha shilingi takribani milioni 8 zikibaki baada kutumia shilingi milioni 414.6.
Naye Mkuu wa mkoa wa Pwani Bw. Aboubakar Kunenge alisema mkoa wa Pwani unajivunia kuwa na viwanda vingi nchini. Lakini hauwezi kujivunia uwepo huo bila kugusia uimara wa viongozi wa TAKUKURU nchini.
"Leo hii mkoa wa Pwani kungekuwa na rindi la rushwa , wawekezaji wasingewekeza Mkoani kwetu. Hivyo tunapozungumzia uwepo wa viwanda vingi ni lazima tusifu kutokomezwa kwa rushwa kunakofanywa na watendaji wa TAKUKURU mkoani kwetu",alisema mkuu wa mkoa wa Pwani.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na kiongozi mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Pwani Bi. Domina Mkama, kiongozi mkuu wa TAKUKURU Chalinze Bi. Crinsesia Swai, mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Bw. Shaibu Ndemanga, watendaji wa TAKUKURU kutoka makao makuu na wa wilaya zote kutoka mkoa wa Pwani.
Wengine ni watendaji wa TAKUKURU kutoka mikoa jirani na mkoa wa Pwani, viongozi wa vyama vya siasa na wa kidini, klabu za TAKUKURU kutoka shule ya sekondari Chalinze na shule ya msingi Kibiki, Taasisi ya sanaa Bagamoyo pamoja na baadhi ya wakaazi wa Chalinze.













Social Plugin