Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWEKEZA SHILINGI BILIONI 500 KUBORESHA RELI YA KATI....'ISAKA' SHINYANGA KUWA KITOVU CHA MIZIGO

Mhandisi wa Miradi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Edwin akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 19, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga 

******
#Rais Samia Aendelea Kuimarisha Miundombinu

#Reli ya Kati kuboreshwa kwa Kiwango Kikubwa

#Mabwawa, Madaraja kujengwa

#Kutoka Makontena 400 Hadi 6,000

# Serikali yatoa Onyo Kali kwa Wahujumu Reli

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza rasmi Awamu ya Pili ya Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya Kati, mradi mkubwa wa kimkakati unaolenga kuhuisha reli ya zamani, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria, pamoja na kuimarisha uchumi wa taifa kwa kuifanya Bandari Kavu ya Isaka mkoani Shinyanga kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji wa Kikanda.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 19, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi wa Miradi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Edwin, mbele ya Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga David Lyamongi, amesema Serikali ya Tanzania imepokea dola za Marekani milioni 200, sawa na takribani shilingi bilioni 500, kwa ajili ya kugharamia shughuli za ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya reli ya zamani.

Mhandisi Edwin amesema reli ya kati ilijengwa tangu enzi za ukoloni na kwa muda mrefu imekuwa chakavu, hali iliyopunguza uwezo wake wa kuhudumia mizigo na abiria kwa ufanisi. 

Amefafanua kuwa awamu ya kwanza ya mradi ilianza mwaka 2014 na kukamilika 2022, hata hivyo haikuweza kufikia malengo yote kutokana na upungufu wa rasilimali fedha, jambo lililosababisha Serikali kuja na awamu hii ya pili yenye wigo mpana zaidi.

Katika awamu hii ya pili, TRC itatekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo utandikaji wa reli kwa takribani kilomita 392, katika kipande cha reli kuanzia Dar es Salaam hadi Isaka. 

Kwa mkoa wa Shinyanga, kazi kubwa zitafanyika katika kipande cha Tabora hadi Isaka, ambapo reli zote chakavu zitaondolewa na kuwekwa reli mpya, nzito na zenye uwezo wa kupitisha treni ndefu na nzito zaidi.
Mhandisi wa Miradi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Edwin.

“Tutafanya pia ukarabati mkubwa wa madaraja 171, ambayo yataongezewa uwezo wa kupitisha maji ili kuondoa changamoto za mafuriko. Aidha, kutakuwa na ujenzi na ukarabati wa mabwawa sita, pamoja na ujenzi wa mabwawa mawili makubwa yatakayojengwa na Serikali kupitia mapato ya ndani. Hivyo, jumla ya mabwawa yatakuwa nane, yatakayotumika kwa umwagiliaji, ufugaji wa samaki na matumizi mengine ya kiuchumi,” amesema Mhandisi Edwin.

Ameongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, TRC itashirikiana kwa karibu na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili kuhakikisha uwekezaji huo unaleta manufaa mapana zaidi kwa wananchi.

Kwa mujibu wa TRC, matokeo ya mradi huu yanatarajiwa kuwa makubwa kiuchumi na kimkakati. 

Kwa sasa, reli ya kati husafirisha wastani wa makontena 400 kwa mwaka kutoka Dar es Salaam hadi Isaka, lakini baada ya kukamilika kwa mradi, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi makontena 6,000 kwa mwaka.
 
Aidha, muda wa upakiaji na upakuaji wa mizigo katika Bandari Kavu ya Isaka utapungua kutoka saa 10 hadi saa 4, kufuatia ukarabati wa miundombinu ya bandari hiyo.

Mhandisi Edwin pia amesema muda wa safari za treni za mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Isaka utapungua kutoka wastani wa saa 50 hadi saa 30, hatua itakayopunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi. 

Vilevile, mradi huu utaongeza njia za kupishania treni ili kuruhusu treni ndefu na nyingi zaidi kufanya safari kwa wakati mmoja.
Mhandisi wa Miradi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Edwin.

Katika hatua nyingine, TRC itafungua milango kwa sekta binafsi, ambapo wawekezaji binafsi wataruhusiwa kuendesha treni zao katika miundombinu ya TRC. Hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya reli, kuongeza idadi ya treni na kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.

Mradi huu umeanza rasmi Machi 2025 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2029, huku huduma za reli zikiendelea kutolewa bila kusitishwa wakati uboreshaji ukiendelea.

 “Tunayo SGR, lakini tumeamua pia kuboresha reli ya zamani ili zote zifanye kazi kwa ufanisi, kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya usafirishaji wa mizigo,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, amesema mkopo wa shilingi bilioni 500 kutoka Benki ya Dunia ni fursa kubwa kwa mkoa wa Shinyanga na taifa kwa ujumla. 
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi

Amesema maboresho ya reli ya kati yataifanya Isaka kutumika rasmi kupokea makontena moja kwa moja kutoka Bandari ya Dar es Salaam, hatua itakayorahisisha nchi jirani kuchukua mizigo yao kupitia Tanzania.

Amewahimiza wananchi wa mkoa wa Shinyanga, hususan Halmashauri za wilaya za Manispaa ya Kahama na Msalala, kutumia fursa za ajira zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi huo, pamoja na kujihusisha na biashara ndogondogo na za kati zitakazohitajika kuhudumia mradi.

 Ameongeza kuwa halmashauri zitanufaika kwa kupata vyanzo vipya vya mapato.

Lyamongi amesisitiza kuwa reli hiyo itaendelea kutoa huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria, huku akionya kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa miundombinu na vifaa vyote.

 “Yeyote atakayejihusisha na vitendo vya hujuma atachukuliwa hatua kali za kisheria, kwa sababu huu ni mradi mkubwa wa kitaifa wenye manufaa makubwa kwa taifa,” amesema.
Mhandisi Dkt. Veronica Mirambo

Katika kutoa mtazamo wa mazingira na jamii, Mratibu wa Masuala ya Mazingira na Jamii wa TRC, Mhandisi Dkt. Veronica Mirambo, amesema TRC itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vijiji husika na vyombo vya habari kuhusu fursa za mradi, tahadhari za kiafya, na namna ya kujilinda dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi mkubwa.
Kamishna Msaidizi wa Polisi Batseba Kassanga

Naye Kamishna Msaidizi wa Polisi Batseba Kassanga, Afisa Polisi Jamii wa Kikosi cha Polisi Reli Tanzania, amesema TRC imejipanga kikamilifu katika suala la usalama wa wananchi, mazingira, miundombinu na mali za mkandarasi, ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa amani na ufanisi.

Mradi huu unaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha miundombinu ya uchukuzi, kuimarisha reli ya kati na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji wa kikanda na kimataifa.
Mhandisi wa Miradi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Edwin akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 19, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Mhandisi wa Miradi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Edwin akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 19, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi akizungumza na waandishi wa habari
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi akizungumza na waandishi wa habari
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi akizungumza na waandishi wa habari

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com