Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MHE. MILLYA ATEMBELEA KITUO CHA UTOAJI HUDUMA KWA PAMOJA CHA NAMANGA


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. James Kinyasi Millya (Mb.) ametembelea Kituo cha Utoaji Huduma kwa Pamoja Mpakani ( One Stop Boarder Post-OSBP ) cha Namanga kilichopo mkoani Arusha Januari 24,2026.

Akitembelea kituoni hapo, Mhe Millya alipokelewa na Meneja wa Mamlaka ya Mapato mkoa wa Arusha Bw. Deogratius Shuma na wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Longido na watumishi wa taasisi 18 za Serikali zinazotoa huduma katima kituo hicho.

Mhe Waziri Milya pia alikutana na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mpakani ikiwemo TAFFA, CHAWAMATA, TCCIA, na Wanawake Wajasiliamali Mpakani.

Ziara hiyo ililenga kujionea hali halisi ya utendaji kazi wa Kituo cha Namanga kwa upande wa Tanzania, kukagua miundombinu ya Kituo na utoaji wa huduma hususan katika uendeshaji wa shughuli za pamoja za Forodha katika mwamvuli wa Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumza na wadau kituoni hapo Mhe. Millya amesema mpaka wa Namanga ni moja kati ya vituo vikubwa na kitovu cha kiuchumi kati ya Tanzania na Kenya kutokana na usafirishaji wa bidhaa za viwandani, mazao ya kilimo, huduma za utalii na muingiliano wa wananchi ki fursa kati ya nchi mbili.

Katika mazungumzo na wadau, Mhe Millya amepokea changamoto zinazokabili ufanisi wa Kituo cha Namanga, aidha wadau wameishukuru Serikali kwa kutembelea kituo hicho na kuonesha imani kubwa katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo na kuboresha miundombinu ili kuleta tija na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com