
Na Bora Mustafa, Arusha .
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amefanya ziara katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) iliyowekewa kambi maalum na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa lengo la kujionea huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wa moyo jijini Arusha.
Katika ziara hiyo , CPA Makalla amezindua rasmi Kitengo cha Dharura katika Hospitali ya ALMC, huku akieleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi ambapo zaidi ya watu 1,200 walikuwa wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Aidha, CPA Makalla amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kuchunguza afya zao mara kwa mara kwa sababu magonjwa mengi hayana dalili za mapema.
Ameongeza kuwa asilimia 32 ya vifo nchini husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo, kisukari na shinikizo la damu, hivyo akahimiza kugundua matatizo mapema kabla hayajawa makubwa.
“Kila binadamu ni mgonjwa mtarajiwa,” amesema Mkuu wa Mkoa CPA Amos Makalla huku akisisitiza kuwa huduma hizi sasa zitawanufaisha si tu wakazi wa Arusha bali pia watalii na wageni kutoka maeneo mbalimbali. Hii ni kutokana na mkataba wa ushirikiano kati ya JKCI na Hospitali ya ALMC ambao utawezesha matibabu ya moyo kutolewa moja kwa moja jijini Arusha.
Aidha, CPA Makalla ameeleza kuwa uwepo wa huduma hizi ni maandalizi muhimu kuelekea mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika Arusha mwaka ujao.
Amebainisha kuwa Arusha ni jiji la kitalii na linahitaji kuwa na miundombinu bora ya afya kwa ajili ya wageni na wakazi wake.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuwa na bima ya afya kwa kila mwananchi bila kujali uwezo wa kifedha, kwani bima ndiyo njia bora ya kupunguza mzigo wa gharama za matibabu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amesema taasisi hiyo imeshatoa huduma katika mikoa zaidi ya 23 nchini, na hii ni mara ya tatu kufika Arusha.
Ameeleza kuwa Hospitali ya ALMC sasa itasimamiwa na JKCI katika kutoa huduma za moyo, ikiwa na vifaa maalum vya kisasa vitakavyosaidia hata wagonjwa walioko nyumbani.
“Dhamira yetu ni kuokoa maisha ya Watanzania kwa kuwafikia wengi zaidi,” amesema Dkt. Kisenge.




Social Plugin