Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAIMARISHA UFUATILIAJI WA HAKI NA MABORESHO YA MAGEREZA

Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Zuberi Homera akiwa katika picha ya pamoja na maaskari wa magereza mkoani Morogoro alipotembelea gereza la mahabusu kujionea kwa ukaribu haki inavyotekelezwa 

Na Mwandishi Wetu Malunde 1-Blog-Morogoro 

Serikali imeendelea kuimarisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa haki katika maeneo ya vizuizi nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda haki za binadamu na kuimarisha utawala wa sheria.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, amefanya ziara katika Gereza la Mahabusu mkoani Morogoro kwa lengo la kujionea kwa karibu namna haki inavyotekelezwa kwa mahabusu na wafungwa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Homera amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha magereza na maeneo yote ya vizuizi yanakuwa na mazingira rafiki yanayozingatia misingi ya haki, utu na usawa. 

Amesisitiza kuwa kulinda haki za wanaoshikiliwa ni msingi muhimu wa mfumo wa haki jinai na ni nguzo ya kudumisha amani na haki katika jamii.

Katika hatua nyingine, Waziri Homera amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuendelea kutekeleza programu za urekebu kwa kushirikiana na mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA), ambapo mahabusu na wafungwa hupatiwa mafunzo ya ufundi stadi. 

Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha kujitegemea kiuchumi na kujiunga upya na jamii kwa tija pindi wanapomaliza adhabu zao.

Aidha, Dkt. Homera amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia kwa kuyapatia magereza vifaa vya TEHAMA ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuboresha usimamizi wa mifumo ya haki. 

Ameongeza kuwa juhudi hizo zinaenda sambamba na mkakati wa kupunguza msongamano magerezani kupitia kuharakisha usikilizwaji wa mashauri, kuimarisha mifumo ya haki, pamoja na kupanua matumizi ya adhabu mbadala.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com