Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AZZA HILLAL AANZA RASMI KAZI ZA UBUNGE ITWANGI, AFANYA SHEREHE MAALUM YA UFAULU WA MIAKA 9 MASUNULA

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad akila chakula cha pamoja na wananchi Jimbo la Itwangi - Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza kwa njia ya Simu na Waziri wa TAMISEM Prof. Riziki Shemdoe.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi, Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, ameanza rasmi majukumu yake ya Kibunge kwa kuwatambua na kuwapongeza walimu, wanafunzi pamoja na jamii ya Masunula walioweka rekodi ya kihistoria ya ufaulu wa miaka tisa mfululizo katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba.

Hatua hiyo imekuja kufuatia matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba 2025, ambapo wanafunzi wote 30 wa Shule ya Msingi Masunula iliyopo Kata ya Usule, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wamefaulu kujiunga na masomo ya Kidato cha Kwanza kwa mwaka wa masomo 2026.

Kati yao, wanafunzi 18 wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za bweni huku wanafunzi 12 wakijiunga na shule za sekondari za kutwa, wote wakipata daraja la “A”.
Sherehe maalum ya pongezi imefanyika leo Jumatatu Januari 5, 2026, katika viwanja vya Shule ya Msingi Masunula na kuhudhuriwa na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, madiwani wa kata za Jimbo la Itwangi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Edward Ngelela, viongozi wa CCM, wenyeviti wa vijiji, maafisa elimu kata, maafisa watendaji wa kata, wazazi, wanafunzi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Azza amewapongeza walimu na wanafunzi kwa juhudi zao, akibainisha kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya nidhamu, bidii na mshikamano mkubwa kati ya walimu, wazazi, viongozi wa kijiji na wanafunzi.

“Heri ya Mwaka Mpya 2026! Leo Januari 5, 2026, nimeanza rasmi kazi ya kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Itwangi. Tumekuja hapa Masunula kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu, walimu waliofanya kazi kubwa na jamii yote kwa ushirikiano wao. Licha ya shule kuwa ya kijijini, imekuwa bingwa wa matokeo ya Darasa la Saba kwa miaka tisa mfululizo. Nimeona ni vyema tufurahi pamoja, tule pamoja na kujumuika pamoja,” amesema Mhe. Azza.
Katika hafla hiyo, Mhe. Azza amekabidhi zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu kwa walimu wa shule hiyo, zawadi kwa wanafunzi wote waliohitimu na kuchaguliwa kujiunga na sekondari, pamoja na kuwathamini wazazi, viongozi wa kata na kijiji kwa mchango wao mkubwa katika mafanikio ya shule hiyo.

Ameeleza kuwa pongezi hizo haziendi mikono mitupu, bali anawapatia zawadi za bahasha kwa Walimu wote 10 wa shule hiyo, vikombe vyenye picha ya Mbunge vikiwa na maandishi ya kuwapongeza, na vikombe pia kwa Serikali ya Kijiji, huku kwa upande wa wanafunzi wote 30 amewapatia “Counter Books” 10 kwa kila mmoja.
Aidha, Mhe. Azza ameshiriki chakula cha pamoja na wananchi waliohudhuria hafla hiyo ikiwa ni ishara ya mshikamano na umoja.

Aidha, amesema mbali na pongezi na zawadi hizo, pia changamoto zote ambazo zinaikabili shule hiyo tayari ameshaziwalisha kwa Waziri wa TAMISEM Prof. Riziki Shemdoe, ambaye pia alipiga simu kwenye hafla hiyo na kuipongeza shule, huku akiahidi kufanya ziara shuleni hapo na kwamba yale yote ambayo Mbunge Azza amemuambia juu ya shule hiyo watayafanyia kazi.
Akizungumza na wananchi wa Masunula kwa njia ya simu, Prof. Shemdoe amesema tayari amepokea taarifa zote kuhusu shule hiyo, akimhakikishia Mbunge Azza na wananchi kuwa serikali ipo pamoja nao na kwamba changamoto zote zilizobainishwa zitafanyiwa kazi.

Prof. Riziki Shemdoe amesema licha ya kutofika katika hafla hiyo kutokana na majukumu ya kikazi, ataweka Shule ya Msingi Masunula kwenye ratiba ya ziara zake atakapofanya ziara mkoani Shinyanga, na kusisitiza kuwa utekelezaji wa ahadi hizo utaonekana kwa vitendo.
“Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu, na ninaamini kupitia Waziri wa Elimu kama alivyoahidi, changamoto za Shule ya Msingi Masunula zitakwenda kutatuliwa. Mimi kama mwakilishi wenu nitaendelea kuwasemea ili kuhakikisha Jimbo la Itwangi linakwenda kung’ara na watoto wetu wanapata ufaulu mzuri katika shule zetu zote,” amesema Mhe. Azza.

Pia ameahidi kuendelea kushirikiana na jamii ya Masunula na Serikali kuboresha miundombinu ya elimu ili kuhakikisha mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi wa Jimbo la Itwangi.
Amewataka Wazazi, Sungusungu, Serikali ya Kijiji, Kamati ya Shule, Viongozi wa Serikali, waendelee kuwa karibu na Walimu na kuzungumza lugha moja ili waendelee kufaulisha wanafunzi kwa ufaulu wa daraja “A” na kwamba shule zingine zinapaswa kuiga mfano huo wa Masunula.

“Shule hii ya Masunula na historia nayo nilishafika hapa mwaka 2017 nikiwa Mbunge wa Vitimaalum, nikiwa na aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga kipindi hicho Jasinta Mboneko na ilikuwa inataka kufungwa sababu ya ukosefu wa choo, nikajenga choo kwa kushirikiana na nguvu za wananchi, hivyo changamoto zote tutazitatua kwa vitendo,” ameongeza Mhe. Azza.

“Nataka kuona shule zote za Jimbo la Itwangi zinafanya vizuri kwenye mitihani ya taifa. Masunula imeonesha mfano, hatuna budi kujifunza hapa”, amesema Azza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Mhe. Edward Ngelela ameipongeza Shule ya Msingi Masunula kwa kuwa mfano wa kuigwa, wakisisitiza umuhimu wa shule nyingine kuja kujifunza mbinu zilizowezesha mafanikio hayo.
Ngelela amepongeza uongozi wa Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal kwa kuipa kipaumbele elimu, akisema jitihada hizo zinaakisi utekelezaji wa Ilani ya CCM ambapo amesisitiza kuwa chama kitaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wananchi katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na endelevu.
Akizungumzia mchango wa halmashauri, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Dkt. Kalekwa Kasanga amesema mafanikio ya Shule ya Msingi Masunula ni fahari kwa halmashauri hiyo, akibainisha kuwa elimu bora ni kipaumbele cha halmashauri huku akiahidi kutuma timu ya wataalamu kufanya tathmini ya changamoto zake ili zitatuliwe.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Seth Msangwa ameipongeza shule hiyo kwa matokeo bora, akisema mafanikio hayo yanadhihirisha umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa serikali, walimu na wananchi huku akiahidi kuwa baraza la madiwani litaendelea kuisimamia sekta ya elimu na kuunga mkono jitihada zote zinazolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Afisa Elimu wa Shule za Msingi wa halmashauri hiyo Andrew Mitumba, amesema Shule ya Msingi Masunula ni jicho la Halmashauri, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, viongozi na walimu uendelee.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Daudi Shineneko, akisoma taarifa ya shule, amesema ilianzishwa mwaka 1977 ikiwa na wanafunzi 80, lakini sasa hivi ina jumla ya wanafunzi 615, pamoja na Walimu 10, Walimu nane walioajiriwa na walimu wawili wa kujitolea.

Amesema shule hiyo imeanza kufanya vizuri katika matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba kuanzia mwaka 2015 na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya kwa miaka 9 sasa, huku malengo yao yakiwa ni kushika nafasi ya kwanza kitaifa.

Amesema katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2025, wanafunzi wote 30 wamepata ufaulu wa Daraja “A”, na wanafunzi 18 wamechaguliwa kwenda shule maalumu za bweni, huku mafanikio hayo yakitokana na ushirikiano wa wazazi, kamati ya shule, sungusungu na viongozi wa serikali ya kijiji.

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kufundisha kwa bidii pamoja na kufanya mitihani ya majaribio mara kwa mara.

Mmoja wa wanafunzi waliofaulu, Sato Salumu, amemshukuru Mbunge Azza kwa msaada wa vifaa vya shule, akisema nidhamu na kusikiliza walimu ndizo siri ya mafanikio yao.

Jamii ya Masunula kupitia kwa mdau wa elimu, Kidamabi Nzegele Manoni imeiomba Serikali kupitia kwa mbunge Azza Hillal kusaidia upatikanaji wa maji kupitia Ziwa Victoria au uchimbaji wa visima virefu ili kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali inayowaathiri katika masomo yao.
"Elimu tunafanya vizuri sana hapa kutokana na ushirikiano tulionao. Sasa nataka nimtumie Mbunge Azza Hillal na Serikali inayoongozwa na ,Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amalize hili tatizo la maji kwa vitendo, hatutaki viongozi wa njoo kesho. Naomba Mbunge ulete maji kwa walimu na wanafunzi wetu tuone mabadiliko",amesema Mzee Manoni.
Shule ya Msingi Masunula ilianzishwa mwaka 1977 ikiwa na wanafunzi 80 pekee, lakini kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 615, wakiwemo wavulana 298 na wasichana 317.

Pamoja na mafanikio makubwa ya kitaaluma, shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa madarasa, upungufu wa walimu, nyumba na vyoo vya walimu, ukosefu wa mabweni, uchakavu wa madarasa, ukosefu wa umeme, vifaa vya michezo pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Mhe. Azza Hillal Hamad akizungumza.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Mhe. Azza Hillal Hamad akizungumza.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Mhe. Azza Hillal Hamad akizungumza.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Mhe. Azza Hillal Hamad akizungumza.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza kwa njia ya Simu na Waziri wa TAMISEM Prof. Riziki Shemdoe.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com