Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAHITIMU MAENDELEO YA JAMII WATAKIWA KUWA CHACHU YA MABADILIKO NCHINI – MHE. MARYPRISCA



Na Jackline Minja WMJJWM- Arusha

Wahitimu wa Kada ya Maendeleo ya Jamii wametakuwa kuwa chachu ya kuleta mabadiliko katika jamii kwa kutumia utaalamu wao kuisaidia jamii kutumia fursa na rasilimali zinazowazunguka kujiletea maendeleo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa Mahafali ya 15, duru ya pili ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru yaliyofanyika tarehe 05 Disemba, 2025 katika Viwanja vya Chuo hicho.

Mhe. Maryprisca amesema mafanikio yatategemea sana bidii, nidhamu, ubunifu, ujuzi, uwajibikaji, uadilifu na uzalendo hivyo amewasihi kuyapa umuhimu ili yakawe nyenzo muhimu katika maisha yao ya kila siku.

“ Niwaambie kwamba mabadiliko haya yanaleta changamoto ambazo hazikuzoeleka awali lakini habari njema ni kuwa yanaleta fursa mpya vilevile naamini kuwa mmeandaliwa vyema na pamoja na kuwa mna maarifa ya kitaaluma, lakini pia mmejengwa kiakili, kitabia na kimaadili kwa hivyo, oneni mabadiliko haya kama fursa za kubuni, kupanga na kutekeleza shughuli mbalimbali kwa mustakabali wenu na Taifa kwa ujumla”. amesema Mhe. Maryprisca.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru aliyemaliza muda wake Dkt. John Elton Lusingu amesema Bodi ya Uendeshaji ni kiungo muhimu katika uongozi wa Taasisi yoyote ya umma na ni chombo chenye wajibu wa kusimamia utekelezaji wa majukumu ya kiutawala, kimkakati na kifedha ili kuhakikisha uadilifu, uwajibikaji na uendelevu wa Taasisi kwa ajili ya kuongeza tija, kuimarisha utawala bora, kuimarisha utendaji na kuchochea kiwango cha utoaji wa huduma.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu ya utumishi wa Bodi, tumepata mafanikio mengi katika maeneo kama vile taaluma, mapato, amani na utulivu, utumishi, utafiti na ushauri elekezi. Nichukue fursa hii kukuomba unifikishie shukrani kwa Mhe. Rais wa kwa kuniamini na kuniteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi.

Kwa niaba ya wahitimu wote Mhitimu aliyefanya vizuri kwa mwaka 2024/2025 Rehema Fisso, wa Shahada ya Awali ya Jinsia na Maendeleo ya Jamii amewashukuru wahadhiri na walezi wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa kuwalea vizuri katika maadili ambayo yatawapa nafasi ya kuishi maisha ya nidhamu wakiwa kazini na katika majukumu mengine ya maisha.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com