Serikali ya Tanzania katika taarifa yake kwa Vyombo vya habari leo Ijumaa Disemba 05, 2025 imetangaza kuzipokea na kuzifanyia kazi taarifa na matamko mbalimbali yaliyotolewa na nchi rafiki, mashirika ya kimataifa na Taasisi za maendeleo kuhusu Tanzania na matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Jumatano Oktoba 29, 2025.
Kulingana na Taarifa ya Wizara ya mambo ya nje, miongoni mwa waliotoa matamko hayo ni pamoja na Ubelgiji, Canada, Denmark, Ujumbe wa Umoja wa Ulaya (EU), Finland, Ufaransa, Ghana, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Poland, Slovakia, Hispania, Sweden, Uswisi, Uingereza, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Marekani pamoja na Taasisi ya Thabo Mbeki ya Afrika kusini.
Katika taarifa hiyo, Tanzania imeonesha kushangazwa na baadhi ya maudhui ya matamko hayo, hasa ikizingatiwa kuwa kulifanyika mazungumzo ya wazi kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi wanaowakilisha nchi hizo nchini, tarehe 28 Novemba 2025.
Serikali imesisitiza kuwa, pamoja na kutambua nafasi ya jumuiya ya kimataifa katika kuimarisha demokrasia na maendeleo ya kijamii na kisiasa, ni muhimu pia kuheshimu uamuzi wa kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi itakayochunguza kwa kina matukio ya vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi, na kuandaa ripoti kamili.
Ripoti hiyo, kwa mujibu wa Serikali ndiyo itakayoleta uelewa mpana kuhusu kilichotokea na kuwa msingi wa mashauriano na ushirikiano wa baadaye katika kujenga taifa lenye amani na umoja.
"Serikali ya Tanzania inaendelea kuwa mstari wa mbele katika ushirikiano wa kimataifa kwaajili ya amani na maendeleo na inatoa wito kwa wadau wote kuruhusu mifumo ya kitaifa kufanya kazi yake kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa," imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, Serikali ya Tanzania imewahakikishia wadau wa maendeleo na jumuiya ya kimataifa kuwa itaendelea kujadiliana na kushirikiana nao katika masuala yote ya maslahi ya pande zote, kwa misingi ya usawa na kuheshimiana.

Social Plugin