Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Chuo Kikuu cha St. John cha Tanzania (SJUT) kimefanya mahafali yake ya 16 katika Kampasi ya Mazengo na kuwatunuku shahada mbalimbali wahitimu 928, ambapo 474 ni wanawake (51.1%) na 454 ni wanaume (48.9%).
Mahafali hayo yamehudhuriwa na viongozi wa mbalimbali, Taasisi za dini, wazazi na wadau wa elimu kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza kwenye mahafali hayo leo Desemba 6, 2025, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Yohana P. Msanjila, amesema mwaka huu chuo kimetoa wahitimu 40 wa shahada za umahiri, 627 wa shahada za awali, 249 wa stashahada na 12 wa astashahada.
Amesema SJUT inaendelea kufanya mageuzi ya kitaaluma ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira na kuandaa wahitimu wenye ujuzi, maadili na uwezo wa kubuni majawabu ya changamoto za jamii.
“Tunajivunia kuandaa wahitimu wenye maarifa, maadili na moyo wa utumishi,tunawaamini kuwa wataenda kuwa mabalozi wazuri wa SJUT katika jamii na kwenye maeneo ya kazi,” amesema Prof. Msanjila.
Amewahimiza wahitimu kutumia uwezo wao kuanzisha miradi bunifu badala ya kutegemea ajira pekee.
“Elimu ya chuo kikuu ni tiketi ya kuingia kwenye dunia ya ushindani,Tanzania inahitaji vijana wenye dira, uthubutu na uwezo wa kutumia teknolojia kutatua matatizo ya jamii,” amesema.
Katika hatua nyingine, Prof. Msanjila ametaja mafanikio ya chuo kwa mwaka wa masomo 2024/2025, ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa maabara tatu za Shule Kuu ya Famasia kwa asilimia 100, ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika mwaka wa masomo 2026 baada ya vifaa kukamilika.
Aidha, amesema chuo kimekamilisha ukarabati wa ukumbi wa mikutano na ujenzi wa kumbi tatu za kisasa kukidhi ongezeko la udahili wa wanafunzi wa programu zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Wahitimu kutoka kozi mbalimbali ikiwemo Afya, Biashara, Sayansi Jamii, Elimu, TEHAMA na Uongozi wametunukiwa shahada, stashahada na astashahada baada ya kukamilisha masomo yao kwa mafanikio.
Miongoni mwa wahitimu hao ni mwanafunzi wa fani ya Famasia,Jonas Musa ambaye amesema safari yake ya elimu SJUT imekuwa yenye changamoto na mafanikio, ikijumuisha mafunzo ya kitabibu, kazi za maabara na mafunzo kwa vitendo yaliyomjengea uelewa mpana wa taaluma hiyo.
Amesema mafunzo aliyopata yamemwezesha kuwa na uwezo wa kitaalamu katika utayarishaji na usimamizi wa dawa, kutoa ushauri kwa wagonjwa na kufanya utafiti mdogo wa kitabibu, akieleza kuwa mazingira ya chuo na walimu wenye weledi vimejenga misingi imara ya taaluma yake.
Mhitimu huyo ameahidi kutumia maarifa yake kuboresha huduma za afya nchini, hususan katika sekta ya dawa na usimamizi wa matibabu.
Pia amewashukuru walimu, wazazi na marafiki kwa mchango wao katika safari ya elimu, huku akihamasisha wanafunzi wengine kujituma na kuchagua fani zenye mchango kwa maendeleo ya taifa.



Social Plugin