Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAASISI 9 WATETEZI WA HAKI ZA KIJAMII ZAUNGANA KUKOMESHA UKATILI WA KIDIJITALI DHIDI YA WANAWAKE NA WASICHANA


Na Maryam Nassor

Taasisi tisa zinazotetea haki za wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na watoto Zanzibar zimeungana kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Udhalilishaji wa Kijinsia, kwa kuweka mkazo kwenye vitendo vya udhalilishaji vinavyofanyika katika mitandao ya kijamii.

Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA ZNZ) zilizopo Tunguu, Unguja.

Akifungua kikao hicho cha tathmini ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Mjumbe wa Bodi ya TAMWA ZNZ, Mwatima Rashid Issa, alisema juhudi zaidi zinahitajika ili kupinga vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto kupitia elimu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.
Amesema kuwa bado jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu matumizi salama ya mitandao, hali inayochangia kuongezeka kwa udhalilishaji dhidi ya wasichana na wanawake, hususan wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi nchini.

“Juhudi zaidi zinahitajika kupinga udhalilishaji kwa wanawake na watoto kwa kuendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii. Hali ni mbaya kwa sasa,” alisema Mwatima.

Aidha, alibainisha kuwa taasisi za kijamii zina nafasi kubwa katika kupinga udhalilishaji kwa kuwa ndizo watetezi wakuu wa haki za wanawake na watoto, hivyo zitaendelea kuhamasisha jamii kushiriki kukomesha vitendo hivyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Sabah Ali Mzee, akisoma tathmini ya uchaguzi iliyoandaliwa na taasisi hizo, aliipongeza Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa mara ya kwanza kuweka takwimu za watu wenye ulemavu katika uchaguzi wa mwaka huu.

Hata hivyo, alisema licha ya hatua hiyo nzuri, changamoto zimeonekana katika baadhi ya vituo vya kupigia kura ambavyo havikuwa na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, hususan wasioona.
Sabah alisisitiza umuhimu wa kutumia siku hizi 16 kupaza sauti dhidi ya udhalilishaji wa watu wenye ulemavu na watoto, hasa unaofanyika katika mitandao ya kijamii.

“Sisi kama JUWAUZA tunapinga vikali tukio lililoonekana mitandaoni likimuonesha mbunge wa viti maalumu (walemavu) akipostiwa vibaya wakati akila kiapo bungeni Dodoma,” alisema.

Amewataka wadau kuungana kupinga udhalilishaji kwa sababu watu wenye ulemavu wana haki sawa na wengine katika jamii.

Naye Wakili na Inspekta wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Sadik Ali Suleiman, alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wanawake na wanaume kutumiana au kurushiana picha chafu, kitendo kinachochochea udhalilishaji mkubwa mtandaoni.

Amesema ni kosa la jinai kutumia mitandao kumtishia mtu au kusambaza picha za ngono, kwani mara nyingi kitendo hicho ndiyo chanzo cha udhalilishaji.

“Ni dhambi kubwa kuwa na picha za ngono katika simu yako. Ikitokea mpenzi wako anakumisi, mwambie akutumie nauli umuone, lakini usitume picha zako,” alitanabahisha Inspekta Sadik.

Ameitaka jamii kushirikiana kupinga udhalilishaji wa aina zote iwe ni ubakaji au udhalilishaji wa kimtandao—kwani vyote ni makosa ya jinai.
Padri Lameck Kiunge kutoka Kanisa la Kilutheri alisema udhalilishaji wa kimtandao kwa sasa umeshika kasi na kuiomba jamii kushirikiana kukomesha ukatili huo.

“Mara nyingi nikiangalia mitandaoni namkuta mwanamke mmoja anawatukana viongozi wa Tanzania. Naumizwa sana na hili, lakini kwa sasa nashukuru kwa sababu amefungiwa,” alisema.
Viongozi kutoka Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), akiwemo Rajab Hamad Abdalla, walisema wataendelea kutoa elimu ya kupinga vitendo vya udhalilishaji katika mitandao ya kijamii.

Washiriki wengine wa kikao hicho wamesema jamii ina jukumu kubwa la kuelimishana kuhusu matumizi salama ya mitandao ya kijamii pamoja na kupinga udhalilishaji dhidi ya wanawake na watu wenye ulemavu.
Jumla ya Taasisi tisa zimeratibu maadhimisho hayo, ambazo ni JUWAUZA, Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Pamoja Youth Initiative (PYI), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), PEGAO, ZAFAYCO, Jukwaa la Vijana Zanzibar (ZYF), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), pamoja na TAMWA ZNZ.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com