SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa elimu kwa wafanyabiashara wa mchele na wamiliki wa viwanda vya kukoboa mpunga katika wilaya za Nzega, Igunga na Tabora zilizopo mkoani Tabora, kuhusu utaratibu wa kupata alama ya ubora kutoka (TBS) Kanda ya Magharibi, hatua inayolenga kuwawezesha kutambulika kitaifa na kimataifa.
Elimu hiyo imetolewa na timu ya maafisa kutoka TBS Kanda ya Magharibi wakiongozwa na Kaimu Meneja, Hamis Seleleko,
Akizungumza katika mafunzo hayo Seleleko amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia wazalishaji wa mpunga ili kuwajengea uelewa juu ya vigezo vya ubora na kuongeza imani kwa walaji.
Amesema umuhimu wa nembo hiyo ya ubora nikuwafungulia fursa wafanyabiashara katika soko huru la Afrika Mashariki kwani inaongeza Imani kwa walaji kuhusiana na ubora wa biordhaa husika.
"Alama ya ubora ni takwa la lazima kisheria kwa bidhaa za chakula na vipodozi kwahiyo tunawasihi wazalishaji bidhaa zao ziwe na nembo ya ubora na wananchi tunawasihi waendelee kutizama bidhaa wanazotumia"Amesema Seleleko.
Mbali na hayo,amesema alama hiyo ya ubora itasaidia katika kukuza uchumi wa mfanyabiashara sambamba na kuchangia kuongeza mapato ya serikali na hivyo kupelekea maendeleo katika jamii.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wa mchele pamoja na wamiliki wa mashine za kukoboa mpunga wilayani Igunga wamesema kuwa kuwa na nembo ya ubora ya TBS kunawaongezea nafasi katika masoko ya kimataifa na kuwasaidia kuuza bidhaa zao kwa uhakika zaidi.






Social Plugin