Serikali imepanga kufanya mageuzi makubwa katika uongozi wa mashirika ya umma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa watendaji wakuu na wajumbe wa bodi za wakurugenzi wanapatikana kwa njia ya ushindani ili kuongeza uwazi, uadilifu na ushiriki mpana wa Watanzania wenye sifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema mfumo huo mpya utaanza kutumika kuanzia Julai 1, 2026 mara baada ya kupitishwa kwa sheria mpya inayoandaliwa na serikali.
Amesema uamuzi huo ni sehemu ya mpango mpana wa kuboresha utendaji wa mashirika ya umma, kuweka uwazi katika uteuzi wa viongozi, na kuondoa utaratibu wa uteuzi wa moja kwa moja uliokuwa ukilalamikiwa na wadau kwa kukosa ushindani wa wazi.
“Kama ni Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO utaomba, uta-apply, na utashindanishwa. Kama unataka kuwa mjumbe wa bodi ya TPA au TISEZA utapitia mchakato wa ushindani. Watanzania wote wenye sifa wataomba, na uchaguzi utafanywa kwa ‘competitive recruitment,” amesema.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Prof. Mkumbo amesema mageuzi hayo yanakwenda sambamba na hatua kadhaa zinazolenga kuongeza tija ya mashirika ya umma na kuimarisha mchango wake katika uchumi wa taifa na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Prof. Mkumbo amesema serikali inaunda mfumo mpya na imara wa kupima maendeleo ya mashirika ya umma kwa kuzingatia tija ya kiuchumi na ubora wa huduma. Mashirika hayo yatapewa vigezo vipya vya kupimwa na kila moja litahesabiwa kwa kiwango kinachochangia kwenye uchumi na ustawi wa wananchi.
Amesema sheria mpya itayataka baadhi ya mashirika ya umma ya kibiashara kujisajili katika Soko la Hisa ili Watanzania waweze kununua hisa na kumiliki mashirika yao, kupanua uwazi katika uendeshaji, na kuongeza uwajibikaji kwa menejimenti na bodi.

Social Plugin