Na Mwandishi wetu, Dar
Serikali imeweka kipaumbele katika kuhuisha majengo na kupanga upya miji mikubwa, hatua inayolenga kuongeza thamani ya makazi, kuboresha matumizi ya ardhi na kuvutia uwekezaji katika kipindi cha pili cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema mpango huo utatekelezwa kwa ubia kati ya wananchi na sekta binafsi kwa lengo la kubomoa nyumba chakavu, kujenga majengo mapya ya ghorofa na kuhakikisha wakazi wanalindwa na kunufaika kupitia upatikanaji wa ‘floor’ za makazi na biashara katika majengo hayo mapya.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam siku ya Jumatatu, Prof. Mkumbo amesema Serikali tayari imeainisha maeneo matatu ya kuanziaVingunguti, Buguruni na Manzese ambapo michakato ya kuwavutia wawekezaji itatangazwa rasmi hivi karibuni. Amesisitiza kuwa wakazi waliopo hawataachwa nyuma, bali watanufaika moja kwa moja katika miradi husika.
Ameeleza kuwa mageuzi ya miji ni sehemu ya mkakati mpana wa kufungua fursa za uchumi, kuongeza ajira na kuboresha ubora wa maisha mijini, akibainisha matumaini ya Serikali kuona miji ya Dar es Salaam na baadaye mingine nchini ikiwa na makazi yaliyopangwa vizuri, miundombinu ya kisasa na mazingira rafiki kwa uwekezaji.
Aidha, sambamba na kuhuisha miji, Serikali inaelekeza nguvu katika kufungua maeneo mapya ya utalii tofauti na yale yanayofahamika sana kama Ukanda wa Kaskazini. Prof. Mkumbo ametaja Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kama eneo kubwa lenye uzuri wa kipekee lakini bado halijatumika kikamilifu. Pia amesema utalii wa fukwe haujanufaishwa vya kutosha licha ya Tanzania kuwa na mwambao mrefu wenye vivutio vingi.
Kwa mujibu wake, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ndani na nje ya nchi ili kuongeza uwekezaji katika utalii, ujenzi na miundombinu, hatua itakayochochea ukuaji wa mapato ya taifa pamoja na kupanua ajira kwa vijana.


Social Plugin