Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI KASPAR MMUYA AFANYA ZIARA YA KIKAZI OFISI ZA WIZARA YA ARDHI DAR ES SALAAM

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, leo tarehe 29 Desemba 2025, amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kukagua utoaji wa huduma na kuzungumza na watumishi wa wizara hiyo kuhusu namna ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, Mhe. Mmuya amewataka watumishi wa Ofisi za Ardhi kuhakikisha wanahudumia wananchi kwa uadilifu, uwazi na kwa wakati unaofaa, huku akisisitiza kuwa sekta ya ardhi ni nyeti sana kwani inagusa moja kwa moja maisha ya wananchi. 

Amesema kuwa sekta hii inapaswa kusimamiwa kwa weledi, haki, na uzingatiaji wa sheria ili kuondoa migogoro ya ardhi na kuhakikisha amani ya wananchi.

“Mwananchi anafurahia kuona anamiliki ardhi yake kihalali, kwa amani na bila migogoro yoyote. Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo vya rushwa, uzembe na uvunjifu wa taratibu katika utoaji wa huduma za ardhi,” amesema Mhe. Mmuya.

Naibu Waziri amezungumzia umuhimu wa sekta ya Ardhi katika mpango wa maendeleo ya Taifa, akibainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipa kipaumbele cha juu sekta hii.

“Sekta ya ardhi ni mhimili wa maendeleo ya kiuchumi, hakuna kilimo, viwanda wala uwekezaji wowote unaoweza kufanikishwa bila ardhi. Hivyo basi, sekta hii inahitaji kuendeshwa kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji wa hali ya juu,” amesisitiza Mmuya.

Mhe. Mmuya  amewapongeza watumishi wa Wizara ya Ardhi kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya, akiwahimiza kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kuongeza uwajibikaji na kuendana na mageuzi ya kidijitali.

Amesisitiza kuwa kuboresha huduma za ardhi kunapaswa kuwa kipaumbele cha kila mtumishi, ili wananchi wapate huduma bora, haraka na kwa urahisi, bila vikwazo vya hila au upendeleo.

Aidha, amehimiza mifumo ya TEHAMA ikiwemo e-Ardhi iendelee kutumika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Dar es salaam ili kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati hatua inayopunguza muda wa wananchi kufuatilia hati badala yake kutumia muda huo kwa shughuli za kukuza mapato yao na taifa kwa ujumla.

Ziara hii ya kikazi imeonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya ardhi inakua kuwa ya kisasa, yenye uwazi, na inayowezesha maendeleo endelevu ya wananchi wote wa Tanzania.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com