Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUU WA WILAYA AZINDUA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE...AHIMIZA ELIMU KWA WANANCHI

Na Bora Mustafa - Arusha

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mheshimiwa Joseph Mkude, leo amezindua rasmi kampeni ya uhamasishaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akibainisha kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora, jumuishi na endelevu za afya.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Mkude amesema mpango huo ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayotekelezwa katika sekta ya afya nchini, yenye lengo la kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wote.

Amesisitiza kuwa bima ya afya si suala la hiari tena bali ni hitaji la msingi kwa maendeleo ya jamii, huku akiwataka viongozi katika ngazi zote kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu sahihi kuhusu umuhimu wa kujiunga na mpango huo mapema.

“Bima ya afya kwa wote si hiari tena, bali ni msingi wa maendeleo ya jamii. Ni wajibu wetu kama viongozi kuwahamasisha wananchi kujiunga mapema ili kujihakikishia usalama wa kiafya,” amesema Mheshimiwa Mkude.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa gharama ya shilingi 150,000 kwa kaya moja kwa mwaka ni nafuu ikilinganishwa na gharama kubwa za matibabu ambazo wananchi wamekuwa wakizilipa hapo awali. 

Ameagiza watendaji wa kata, mitaa pamoja na mabalozi wa nyumba kwa nyumba kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wananchi wote bila ubaguzi.

Kwa upande wake, Afisa Uanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Miraji Kisile, amesema mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unatarajiwa kuzinduliwa rasmi kitaifa mwezi Januari 2026. Ameeleza kuwa mpango huo utawawezesha wananchi kupata huduma za afya bila vikwazo vya kifedha katika vituo vya afya vya serikali na binafsi vilivyosajiliwa.

Kisile amesema michango ya wanachama itagharamia huduma mbalimbali zikiwemo vipimo, matibabu, dawa, kulazwa na upasuaji. Amefafanua kuwa bima hiyo imelenga kaya zenye watu wasiozidi wanne, wakiwa na umri chini ya miaka 21.

Ameongeza kuwa huduma za bima hiyo zitapatikana katika hospitali na vituo vya afya vilivyosajiliwa na NHIF nchi nzima, ikiwemo hospitali za serikali, za taasisi za dini na sekta binafsi.

Naye Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Julius Sekeyani, pamoja na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Wilfred Soilei, wameeleza kuwa ushirikiano wa viongozi wa mitaa na kata ni nguzo muhimu katika kufanikisha elimu ya bima ya afya kwa wote.

Viongozi hao wamesisitiza kuwa uhamasishaji wa afya kwa wote utaongeza uelewa wa wananchi na kuleta ushiriki mpana wa jamii katika kuimarisha ustawi wa afya.

Kwa pamoja, wamewataka wananchi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa hiyo, wakibainisha kuwa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni hatua muhimu kuelekea upatikanaji wa huduma bora, nafuu na jumuishi za afya kwa kila Mtanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com