Tanzania imejikuta katikati ya vuta nikuvute ya kidiplomasia kufuatia matamko na hatua za baadhi ya nchi washirika wa maendeleo baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025. Huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa Tume ya Uchunguzi kutoa majibu sahihi, hatua ya baadhi ya mataifa kutishia au kukata misaada inazua mjadala mzito kuhusu uhuru wa nchi kujitathmini na tabia ya mataifa rafiki kutaka kuingilia masuala ya ndani.
Mchambuzi mashuhuri wa siasa na jamii, Maggid Mjengwa, anatoa nuru mpya juu ya hatua za Sweden, akibainisha kuwa uamuzi wa kukata misaada kwa Tanzania na nchi nyingine tano (ikiwemo Msumbiji na Zimbabwe) haukutokana na matukio ya hivi karibuni, bali ni suala la kiitikadi na maslahi ya kitaifa ya Sweden.
"Ilitarajiwa na haitokani na matukio ya hivi karibuni nchini Tanzania," anasema Mjengwa. "Sababu ya msingi ya kuifutia misaada Tanzania ni Sera za Kijamaa. Tatizo ni Ujamaa wa Tanzania."
Mjengwa anasema wazi kwamba Serikali ya sasa ya Sweden, yenye mrengo wa Kihafidhina, inachukia Sera za Kijamaa za Tanzania zilizowekwa tangu 1962. Kinachoshangaza zaidi, fedha hizo sasa zimeelekezwa Ukraine, ikithibitisha kwamba misaada inafuata vipaumbele vya usalama na maslahi ya taifa la mtoaji (Sweden), na siyo umaskini wa mpokeaji.
Hatua hii ya Sweden na matamko ya baadhi ya nchi za Magharibi kuhusu matukio ya ndani ya Tanzania, yanaibua swali la msingi: Je, misaada ya maendeleo ni kweli kusaidia umaskini, au ni njia ya kuingiza ajenda za kisiasa?
Inaonekana kuna tabia inayoendelea ya mataifa rafiki kutaka kuweka viwango vya maadili vya juu zaidi kwa nchi zinazoendelea kuliko vile wanavyojiwekea wao wenyewe. Matamko yanayotolewa baada ya matukio kama yale ya Oktoba 29 yanaonekana kuwa na lengo la kuishinikiza Serikali kufanya maamuzi yanayokidhi matakwa ya kigeni, badala ya kuheshimu mchakato wa uchunguzi wa kitaifa.
Kwa upande mwingine, Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa inatambua mchango wa washirika wa kimataifa katika demokrasia, lakini imewataka wadau wote kusubiri matokeo rasmi ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa kwa kuwa Tanzania ni nchi ina haki kamili ya kutumia mifumo yake ya kisheria na kitaasisi kujichunguza yenyewe kabla ya kupokea hukumu za nje. Pia mahusiano ya kimataifa yanapaswa kuendelezwa katika msingi wa heshima ya usawa, na si uhusiano wa mtoaji na mpokeaji wa amri.
Kama Mjengwa anavyokumbusha, Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitupitisha kwenye njia ya Ujamaa na Kujitegemea ambayo ilitupa uwezo wa kujihami kiitikadi. Hotuba ya Rais, wakati akifungua Bunge, zimethibitisha hali hii ya majaribu kwa kutoa wito kwa Watanzania kujifunga vibwebwe.
Wito wa kiongozi wa nchi wa kusisitiza kuwa matajiri wanakata misaada unaakisi maono ya zamani ya Nyerere. Ujumbe wake ni wazi: Taifa linapaswa kuzunguka bendera ya Taifa na kulinda umoja wake dhidi ya mbegu za utengano, kwani hakuna nchi nyingine ya kukimbilia.
Ni wakati sasa, kama Mjengwa anavyohimiza, kwa Watanzania kufanya Tafakuri Jadidi juu ya mwelekeo wa Taifa letu. Uhuru wa kutoa maamuzi bila kushinikizwa na misaada ndiyo kiini cha uhai na utambulisho wetu kama Taifa huru.

Social Plugin