JESHI la Polisi nchini limetoa onyo kali na la wazi kwa wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu na uharibifu kwa kisingizio cha ‘maandamano ya amani yasiyo na kikomo’ kuanzia tarehe 9 Desemba 2025. Kwa mujibu wa Jeshi hilo, uhamasishaji huu unalenga kuvuruga amani na maisha ya wananchi.DCP David Misime, Msemaji wa Jeshi la Polisi, amethibitisha kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama vinafuatilia kwa karibu mipango hii hatarishi. Jeshi linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda maisha na mali, huku likiimarisha hali ya amani, utulivu na usalama nchini.
Taarifa ya Jeshi la Polisi inaonyesha kuwa uhamasishaji unaoendelea katika makundi sogozi unalenga kufanya vitendo vitakavyosimamisha nchi na kuingiza taifa katika machafuko:
Wahamasishaji wanawataka washiriki kuharibu na kuchoma moto minara yote ya mawasiliano ili nchi nzima ikose mawasiliano. Pia, wanapanga kufunga Bandari ya Dar es Salaam kwa kuzuia barabara zote za kuingia na kutoka bandarini, hivyo kuzuia shughuli za kiuchumi.
Mipango inahusisha pia kufunga mipaka yote ya nchi ili kuzuia mtu yeyote asitoke au asiingie nchini. Jambo linalotia hofu zaidi ni kwamba wahamasishaji wanahamasishana siku hiyo waende hospitalini kuzuia huduma kwa wagonjwa zisitolewe, kwa lengo la kulifanya Taifa lisimame kabisa.
Kwa upande wa usalama wa raia, uhamasishaji unawataka vijana wakapore mali za watu kwa kisingizio kuwa wana njaa. Pia, kuna matamko kwamba watakwenda kuwafuata watumishi wa Serikali popote walipo ili kuwadhuru. Wakati wa uhamasishaji huo, viongozi wa maandamano hayo wanaelekeza kwamba ambaye hajui kutumia silaha na hajapitia mafunzo siku hiyo asishike silaha, awaachie waliopata mafunzo ya matumizi ya silaha.
Katika kukabiliana na miito hiyo ya uharibifu, Jeshi la Polisi linawapongeza na kuunga mkono wananchi na vijana wanaopenda amani ambao tayari wameahidi kulinda amani katika maeneo yao.
Amani siyo maneno ni kazi. Vijana, kama walinzi wa Taifa, wanahimizwa kukataa kuwa vibaraka wa kisiasa. Katika matamko yanayopinga vurugu, wengine wameapa na kutamka kuwa watakaokwenda kuandamana wasifike kwenye mitaa yao kwani watawashughulikia ipasavyo. Wengine wanasema hawatakubali tena kupata hasara waliyoipata Oktoba 29 na siku zilizofuata, hivyo watahakikisha kuanzia Desemba Tisa wanalinda maisha, familia, na mali zao.
DCP Misime amewahakikishia wananchi wote wapenda amani kuwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vipo tayari kulinda maslahi ya Taifa. Wale wote wanaohamasisha vurugu watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wananchi wamekumbushwa kuwa mwezi huu wa Desemba ni kipindi cha maandalizi ya sherehe za mwisho na mwanzo wa mwaka. Jeshi linawahimiza wananchi kuendelea na maandalizi mazuri yanayozingatia usalama wa maisha na mali zao, na wanahimizwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Amani na Utulivu wa Tanzania utaendelea kuimarishwa, na hakuna mwananchi atakayeruhusiwa kusumbuliwa katika shughuli zake za kila siku.
Social Plugin