Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MEYA WA JIJI LA ARUSHA AELEZA MAFANIKIO YA MIRADI YA MAENDELEO


Na Bora Mustafa  - Arusha

Meya wa Jiji la Arusha, Mhe. Maxmillian Matle Iranqhe, amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jiji hilo umefikia hatua nzuri, huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Silas Shemdoe, akieleza kuridhishwa kwake baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Desemba 18, 2025 Meya Maxmillian amesema Waziri Prof. Riziki ametembelea miradi mbalimbali ikiwemo uwanja wa michezo na soko la Kilombero, ambapo ameshuhudia hatua kubwa ya utekelezaji na kutoa maelekezo ya kuimarisha usimamizi ili miradi ikamilike kwa wakati.

Meya amesema Waziri huyo amesisitiza kuwa hakutakuwa na nyongeza ya muda kwa miradi inayoendelea, akiwataka wakandarasi na wasimamizi kuzingatia mikataba na ratiba ya utekelezaji, ili miradi ikabidhiwe kwa wananchi kwa wakati uliopangwa.

Aidha, Meya Maxmillian amemshukuru Waziri Prof. Riziki kwa kuwapa moyo viongozi wa jiji hilo na kutambua juhudi zinazofanywa katika kusimamia maendeleo. Pia amempongeza Mbunge wa Jiji la Arusha, Mhe. Paul Makonda, kwa mchango wake katika kuhamasisha na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa karibu.

Kwa upande mwingine, Meya amesema mradi wa ujenzi wa stendi mpya ya mabasi ulianza rasmi mwezi Juni mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka ujao. 

Hata hivyo, amesema kutokana na kasi ya ujenzi inayoendelea, kuna dalili nzuri za mradi huo kukamilika kabla ya muda uliopangwa.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wa Jiji la Arusha kuboresha huduma kwa wananchi, kuimarisha miundombinu na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com