Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwassa, amesema majanga mbalimbali yaliyoikumba mkoa huo katika vipindi vya nyuma yamechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa uchumi na kuuchelewesha mkoa huo katika maendeleo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha la Ijuka Omuka, uliofanyika leo Desemba 18, 2025 katika ukumbi wa KCU, Manispaa ya Bukoba, RC Mwassa amesema Mkoa wa Kagera umepitia majaribu mazito yaliyosababisha kusuasua kwa maendeleo ya kiuchumi, lakini pia umejifunza umuhimu wa kudumisha amani na mshikamano.
Amesema ni muhimu Watanzania kutambua kuwa Kagera ni mkoa unaothamini amani, akisisitiza kuwa mkoa huo ndio uliowahi kuonja machungu ya uvunjifu wa amani wakati wa Vita vya Kagera, hivyo una wajibu wa kuwa mfano wa kuhubiri na kulinda amani.
“Wanakagera tumepitia magumu mengi, na majanga hayo ndiyo chanzo cha kurudi nyuma kiuchumi na kutulazimisha kupambana kwa nguvu zaidi kusonga mbele,” amesema RC Mwassa.
Akitaja baadhi ya majanga yaliyoupata mkoa huo, RC Mwassa amesema Vita vya Kagera, janga la ugonjwa wa UKIMWI, ajali ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba, pamoja na majanga mengine, yamesababisha kudorora kwa uchumi wa mkoa huo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa hakuna sababu ya kuingia katika migogoro mipya kwa namna yoyote.
Amehimiza wananchi kudumisha umoja na mshikamano, akisema umoja ndio msingi wa maendeleo, na kuwataka wananchi kuepuka migawanyiko isiyo na tija kwa misingi ya ukabila au dini.
“Inapendeza sana kuona watu wa dini tofauti wakiwa pamoja; kwaya ya kanisani ikiimba, Sheikh akitoa dua, ngoma za asili zikapigwa na Padre akabariki. Huo ndio uzuri na nguvu ya Kagera,” amesema RC Mwassa.
Tamasha la Ijuka Omuka limefunguliwa rasmi leo, Desemba 18, 2025, kwa sala na dua kwa ajili ya Taifa na Mkoa wa Kagera, huku kilele chake kikitarajiwa kufanyika Desemba 21, 2025. Lengo kuu la tamasha hilo ni kuwakutanisha Wanakagera wanaoishi ndani na nje ya mkoa ili kuimarisha umoja na mshikamano.
Aidha, tamasha hilo linalenga kuutangaza Mkoa wa Kagera kiuchumi kwa kuonesha fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo, ikiwa ni pamoja na kongamano la uwekezaji litakalofanyika Desemba 19, 2025, likiongozwa na mgeni rasmi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Vijana.
Kwa upande wa michezo, kutafanyika bonanza maalumu la michezo litakalohusisha makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha afya, urafiki na mshikamano.
Bonanza hilo litafanyika Jumamosi, Desemba 20, 2025, katika Uwanja wa Kaitaba, likijumuisha mechi kati ya makundi mbalimbali ikiwemo machinga na maafisa biashara, waandishi wa habari na walimu, wafanyabiashara na TRA, viongozi wa dini na wakuu wa wilaya, pamoja na mechi ya bodaboda dhidi ya Jeshi la Polisi, ambapo washindi watapewa vikombe.
Tamasha hilo pia litapambwa na maonesho ya ngoma za asili, onyesho la sanaa ya maigizo (amari), simulizi la historia ya Mkoa wa Kagera ikiwemo kuanguka na kuinuka kwa ngome ya Buhaya, maonesho ya machifu pamoja na vyakula vya asili.
Kaulimbiu ya Ijuka Omuka 2025 ni: “Wekeza Kagera, Irudishe Katika Ubora Wake.”














Social Plugin